HIMID Mao, nahodha msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, anayekipiga ndani ya Klabu ya ENPPI ya nchini Misri, jana alitimiza siku ya 26 akiwa amejifungia ndani ya nyumba kutokana na kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Ligi nyingi duniani zimesimamishwa ili kupisha maambukizi zaidi ya Virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia kwa sasa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Himid alisema: “Huku tunashinda ndani ili kupisha maambukizi ya Corona na kuhusu mazoezi pia ninafanya ndani kwani siwezi kutoka nje ilihali hakuna ruhusa ya kutoka kwa sasa.
“Nakumbuka Machi 12 ligi ilisimamishwa na tukaambiwa tushinde ndani ya nyumba, ni janga la dunia kwa sasa lazima tuchukue tahadhari ili kubaki kuwa salama, tulipewa muda wa kufanya manunuzi ya chakula ambacho nami nilijiwekea ndani.”
Lunyamadzo Mlyuka, Dar es Salaam
