×

Yanga Ndiyo Wanaomfanya Manara Atambe

 

KUREJEA kwa Ligi Kuu Bara, mambo mengi nayo yamerejea kwelikweli. Tuliyamisi kwa takribani miezi miwili na nusu.

Zile pilikapilika na maneno ya kuudhi kutoka upande mmoja wa timu kwenda mwingine, zimeanza tena kwa kasi ya ajabu sana.

Ishu za wachezaji, makocha na viongozi kuvurugana, tumezishuhudia tena mapema tu. Naam hii kweli inamaanisha ligi imerejea.

Kabla ya ligi hiyo kusimama, mambo mengi ya aina hiyo tuliyashuhudia. Kusimama kwa ligi tukayakosa, sasa yamerejea tena.

Kadiri siku zinavyozidi kwenda, tumeona namna ambavyo Yanga maisha yao yanavyokwenda. Yanashangaza kwelikweli. Kuanzia kwa viongozi, wachezaji hadi wanachama ambao ndani yao kuna mashabiki. Wote wanashangaza.

Ngoja leo tuwajadili kidogo Yanga kulingana na ukubwa wao na mambo wanayoyafanya ambayo hayaendani na huo ukubwa wao kiasi cha kumfanya Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aendelee kutamba.

Kabla hatujaenda mbali, nikwambie tu kwamba, kutamba kwa Manara kunasababishwa na Yanga wenyewe. Nadhani hawalitambui hilo.

Yanga wanajiita mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara. Wamekuwa wakijivunia hilo, acha wajivunie kwa sababu ukweli uliowazi ni kwamba, ndiyo wanaoongoza kwa kutwaa mara nyingi taji hilo. Mara 27. Hakuna timu nyingine iliyowazidi.

Lakini historia hiyo kama hawajajipanga vizuri, inaweza kufutika haraka kwa sababu kila siku nikiiangalia timu yao inavyoendeshwa, naona wanarudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Nikurudishe nyume kidogo. Kuna wakati wakongwe wenzao kwenye soka la Bongo, Simba nao walikuwa kwenye maisha haya ambayo Yanga bado wanayaishi.

Zamani Simba wanaweza kuishi kwenye mgogoro muda mrefu, Yanga wao wanakula bata tu. Wakati mwingine kibao kinabadilika. Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya hizi klabu mbili kongwe katika soka letu.

Baadaye Simba wakabadilika kabisa, hii ni baada ya kuingia kwenye mfumo wa mabadiliko ambapo hivi sasa ishu zile za migogoro kama ilivyokuwa zamani, haipo. Mchezaji ukizingua, unawekwa pembeni. Wanaoiheshimu kazi yao wanacheza.

Wakati ule kabla mambo hayajawa hivi, Emmanuel Okwi na Juuko Murshid wakienda kwao Uganda walikuwa wakiwasumbua sana kurudi kambini. Hivi sasa mambo hayapo hivyo.

Wachezaji wanaiheshimu klabu na wao wanaheshimika, maisha yanaenda vizuri kabisa.

Lakini kwa wenzao Yanga, bado wanayaishi yale maisha ambayo hawapaswi kuishi kutokana na ukongwe na historia yao wanayoendelea kutamba nayo.

Juzi kati walianza na ishu ya Kocha Luc Eymael kuchelewa kurudi. Kocha anasema hivi, viongozi wanasema vile. Mwisho wa siku kocha amerudi, hakuna kiongozi aliyekwenda kumpokea uwanja wa ndege. Inashangaza sana.

Wakati kocha akiwa njiani kutoka Ubelgiji kurudi Tanzania, huku timu inajiandaa kwenda Shinyanga kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui.

Sakata la kocha likiwa halijapoa, wachezaji wanaibuka na lao jambo. David Molinga na Bernard Morrison ambao ni wachezaji wa kimataifa. Hawasafiri na timu.

Nadhani wote tunafahamu kile kilichotokea katika sakata la Molinga, ilisemekana kwamba mchezaji haelewani na Kocha Msaidizi, Charles Mkwasa.

Sasa kama kocha na mchezaji hawaelewani, wanawezaje kukaa sehemu moja na kufikia malengo ya klabu. Hapo lazima mmoja apishe, ili mambo yaende sawa.

Huku nyuma anakuja Eymael, anamchukua Molinga, wanakwea ndege kuwafuata wenzao waliotangulia na basi la timu. Imenifikirisha sana hii ishu.

Mchezaji ambaye tulielezwa aligoma kusafiri na wenzake kwa njia ya barabara, amekubali kuondoka ‘kibosi’ na kocha kwa kutumia njia ya anga. Wale wengine wanajisikiaje!

Mambo kama haya mwisho wa siku yanashusha morali ya timu. Baadhi ya wachezaji wanajiona hawana thamani kushinda wenzao. Ikifikia hatua hiyo, suala la mafanikio mtalisikia kwenye vyombo vya habari tu.

Kama Yanga wasipobadilika mapema kama wenzao walioamua kubadilika, basi ile kauli ya Manara kwamba watachukua taji la ligi mara tano mfululizo inaweza kutimia na kuzidi kumfanya jamaa huyo mwenye maneno mengi azidi kutamba.

Leave a Comment