
CLATOUS Chama, kiungo bora wa msimu wa 2019/20 anayekipiga ndani ya Klabu ya Simba leo kwenye kilele cha Tuzo za VPL zinazofanyika Ukumbi wa Mlimani City amesepa na tuzo binfasi mbili.
Tuzo ya kwanza ilikuwa ni ya kiungo bora baada ya kuwashinda, Lukas Kikoti wa Namungo na Mapinduzi Balama wa Yanga.
Ameibuka kuwa mchezaji bora kwa msimu wa 2019/20 akiwashinda Nicolas Wadada wa Azam FC ambaye mkononi ana tuzo ya beki bora wa msimu wa 2019/20 na beki wa Coastal Union Bakari Mwamnyeto wote wamo kwenye kikosi bora cha msimu wa 2019/20

Chama ni namba moja kwa pasi za mwisho ndani ya Simba akiwa ametoa jumla ya pasi 10 za mabao huku akifunga mabao 2 na kumfanya ahusike kwenye jumla ya mabao 12 kati ya 78 yaliyofungwa na Simba.
Chama amewapiku beki Bakari Mwamnyeto aliyesaini Yanga akitokea Coastal Union ya Tanga na Nicolas Wadada wa Azam.
Mbali na mchezaji bora Chama amechukua tuzo ya kiungo bora akiwashinda Lucas Kikoti wa Namungo na Mapinduzi Balama wa Yanga.

Tuzo ya beki bora imeenda kwa Nico Wadada wa Azam FC akiwashinda David Luhende wa Kagera Sugar na Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union.
Kwa upande wa Simba tuzo nyingine waliyojinyakulia ni tuzo ya kipa bora aliyochukua Aishi Manula akiwashinda Daniel Mgore wa Biashara United na Nouridine Balora wa Namungo.
Simba iliendelea kung’ara baada ya kocha wao Sven Vandebroeck kutangazwa kuwa kocha bora akiwashinda Hitimana Thiery wa Namungo na Aristica Cioba wa Azam FC.

Tuzo ya mchezaji bora chipukizi ilienda kwa Novatus Dismas wa Biashara United ambaye kawashinda Kelvin Kijiri wa KMC na Dickon Job wa Mtibwa Sugar.
Kwa upande wa mwamuzi bora mshindi ni Ramadhan Kayoko aliyekuwa pilato wa 4-1 za Simba dhidi ya Yanga kwenye mechi ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho Azam (ASFC) ambayo Simba ilichukua kombe hilo kwenye fainali dhidi ya Namungo kwa kuichapamabao 2-1.
Tuzo ya heshima ilienda kwa Sunday Manara aliyewahi ichezea Yanga pia alipata kitita cha Sh3 milioni na anatambulika kama mchezaji wa kwanza Mtanzania kwenda kucheza Ulaya.

Klabu za Simba, Yanga, Azam na Namungo zimepewa tuzo ya timu nne bora huku timu yenye nidhamu ikipewa Kagera Sugar na mfungaji ni Meddie Kagere wa Simba aliyemaliza na mabao 22.
Kikosi Bora
Na hiki ndio kikosi bora cha msimu wa 2019/20 huku Simba wakitoa wachezaji sita kilichotangazwa katika tuzo hizo; golini Aishi Manula (Simba) , mabeki Nico Wadada (Azam), David Luhende (Kagera Sugar) Bakari Mwanyeto (Coastal Union), Sergie Wawa (Simba), viungo Zawadi Mauya (Kagera Sugar), Lucas Kikoti (Namungo), Clatous Chama (Simba). Na washambuliaji ni Meddie Kagere (Simba), John Bocco (Simba), Luis Miquissone (Simba)