
Jumla ya vijana 1191 wamemaliza mafunzo yao ya ufundi stadi ambayo wameyapata katika taasisi ya Don Bosco iliyopo Oysterbay ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Mahafali hayo yamefanyika Oktoba 2 mwaka huu ambapo vijana hao wamepata fursa ya kupata mafunzo hayo ambayo yatawawezesha kuajiriwa au kujiajiri.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo mkurugenzi na mkuu wa chuo cha Don Bosco Oysterbay, Mh.Fr Babu Augustine, amesema kuwa anaishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kuwa mewafanya vijana kupata mafunzo hayo.
“Taasisi ya Don Bosco Networks Tanzania iliingi ubia na Wizara ya kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu ili kutoa mafunzo yanayolenga kukuza ujuzi wa vijana wa Kitanzania kwa njia mbalimbali uanagenzi, mafunzo ya vitendo mahali pakazi na utambuzi wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo.
Katika awamu hii ya pili ya mafunzo haya Don Bosco kushirikiana na VETA kwa pamoja waliweza kutengeneza mtaala wa mafunzo ya muda mfupi unaoendana na mahitaji ya soko la Ajira na mahitaji ya vijana sambamba na kuwajengea uwezo walimu kutoka vyuo washiriki na uboreshaji wa miundo mbinu ya kujifunza na kufundishia.
“Mafunzo ambayo wameyapata ni Useremala, ufundi bomba, uchomelaji na uungaji vyuma, uashi, utengenezaji wa kompyuta, uchangaji wa vipuri, kubuni mitindo ya mavazi, ushonaji na ufundi magari, umeme wa majumbani na viwandani, ufungaji umeme wa jua, mapishi na usindikaji wa chakula, uwekaji terezo na marumaru, ufugaji, kilimo cha mbogamboga, utengenezaji wa samani kwa kutumia alminium na uchapaji wa nyaraka.

“Kwa hiyo napenda kutoa kutoa shukrani za dhati kwa Raisi wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu kwa kutoa fursa hii kwa vijana kwa kuwa wengine waliokuwa hawana uwezo wa kusoma na walikata tamaa lakini sasa wamepata elimu bure kabisa kupitia Serikali hii ya Awamu ya Tano, “amesema.
Nae Program meneja wa Don Bosco Networks Rosemary Njoki ameishuru Serikali kwa ajili ya kushirikiana nao katika kuwapa elimu vijana hao.
“Naishukuru Serikali kwa sababu imejitolea kuwasaidia vijana ambao pengine ndoto yao ilishapotea lakini kupitia masomo hayo vijana hawa wamenufaika kwa kupata ujuzi pamoja na elimu ambayo itakwenda kuwasaidia kwa sababu walikuwa nyumbani wengine walikuwa na changamoto kifedha kupitia Serikali wamepata mafunzo haya ndani ya miezi sita na wamefuzu vizuri”. Alimaliza kusema.