
LICHA ya ugumu wa ratiba yao kwenye michezo mitatu ijayo ya Ligi Kuu Bara, uongozi wa Klabu ya Yanga umesema kuwa ratiba hiyo haiwezi kuwa kikwazo cha kuharibu hesabu zao za kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.
Michezo mitatu ijayo ya Yanga ni dhidi ya Namungo, Azam na JKT Tanzania ambapo dhidi ya timu hizi msimu uliopita Yanga ilishinda mchezo mmoja pekee kati ya sita, ikifungwa mchezo mmoja, huku michezo yote minne iliyosalia ikiisha kwa matokeo ya sare.
Yanga itaanza kibarua dhidi ya Namungo Novemba 22, huku ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare mbili msimu uliopita, mchezo wa kwanza ukiisha kwa sare ya bao 1-1 Machi 15 kabla ya kupata tena sare ya mabao 2-2 Juni 24.
Novemba 25, Yanga itacheza na Azam, msimu uliopita mchezo wao wa kwanza uliisha kwa Yanga kupewa kipigo cha bao 1-0 Januari 18, huku mchezo wa raundi ya pili uliopigwa Juni 21, ukiisha kwa suluhu. Yanga itamalizia dhidi ya JKT Tanzania ambapo msimu uliopita ilishinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-2 Novemba 22, huku mchezo wa marudiano uliopigwa Juni 17, ukiisha kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa kikosi cha klabu ya Yanga, Hafidh Saleh alisema ni kweli ratiba ya michezo yao mitatu ijayo inaonekana kuwa ngumu lakini haiwezi kuwaondolea plani za ubingwa walizonazo.
“Ni kweli ukiangalia ratiba ya michezo yetu mitatu ijayo inaonekana kuwa ngumu ambapo Novemba 22, tutacheza nyumbani dhidi ya Namungo, siku tatu baadaye yaani Novemba 25, tutacheza ugenini dhidi ya Azam kabla ya kurejea nyumbani kumalizana na JKT Tanzania.
“Lakini licha ya ratiba hiyo kuonekana kuwa na ugumu kwetu, niwatoe hofu mashabiki wetu kuwa bado haiwezi kuharibu malengo ambayo tumejiwekea ya kuhakikisha tunatwaa pointi tatu kwenye kila mchezo, ili kurejesha taji la ubingwa tulilolikosa kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita,” alisema Saleh.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 24 walizokusanya kwenye michezo yao 10 waliyocheza.
Joel Thomas, Dar es Salaam