
MTENDAJI Mkuu wa Simba (C.E.O), Barbara Gonzalez, amekiri kuwa timu yao ilistahili kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United kutoka nchini Nigeria huku akikiri kufurahishwa na viwango walivyoonyesha wachezaji wa timu hiyo.
Simba katika michuano hiyo, imefanikiwa kusonga mbele ambapo baada ya kuwaondoa Plateau, wanatarajiwa kukutana na Platinum FC ya Zimbambwe ambayo anachezea mshambuliaji Mtanzania Elias Maguri. Mechi ya kwanza itacheza kati ya Desemba 22-22, mwaka huu na ya marudiano itakuwa kati ya Januari 5-6, mwakani.
Akizungumza mara baada ya timu hiyo kusonga mbele, Barbara alisema kuwa kutokana na upambanaji wa wachezaji waliouonyesha katika michezo yote miwili waliyocheza dhidi ya Plateau United, walistahili kusonga mbele huku akisema kuwa wana timu nzuri ya kupambana.
“Timu imepambana kuhakikisha tunasonga mbele, viwango vya wachezaji wetu walivyoonyesha jinsi gani walihitaji matokeo mazuri, wamecheza vizuri na kwa moyo wao wote na kwa upande wangu naamini Simba tuna timu nzuri ya kupambana katika michuano hii.
“Malengo yetu ni kusonga mbele zaidi ya hapa tulipo kwa sasa, hivyo bado tuna safari ndefu zaidi ya kuhakikisha tunafikia malengo yetu, tunashukuru kwa kufanikiwa kupita katika hatua hii ya kwanza, naamini tutazidi kufanya vizuri huko mbeleni,” alisema kiongozi huyo.
Marco Mzumbe, Dar es Salaam