×

Tanapa Inavyokabiliana na Changamoto Katika Sekta ya Uhifadhi

 

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (Tanapa), limejipangia mikakati ya mazao ya utalii ili kuhakikisha linatekeleza kwa kishindo Ilani ya chama tawala – sekta ya utalii kufikisha watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, kutoka idadi ya milioni 1.5 waliofikiwa kuanzia baada ya uhuru hadi sasa.

 

Ilani hiyo, inaelekeza pia kuwa mapato ya utalii yanatakiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 2.6 (zaidi ya Sh trilioni 6) hadi dola bilioni 6 (karibu Sh trilioni 14) ifikapo mwaka 2025.

 

Changamoto hiyo ni kubwa katika sekta ya utalii lakini Tanapa kwa upande wao wameshaeleza mikakati ya kufikia mafanikio hayo. Ujangili ni tatizo kubwa kwa Tanapa katika kufikia malengo yake. Tanapa iliyoanzishwa mwaka 1959, inasimamia hifadhi 22 zilizopo katika kanda za Mashariki (hifadhi 4), Magharibi (10), Kaskazini (5) na Kusini (3).

 

Katika hotuba yake aliyoitoa jijini Dodoma hivi karibuni akifungua mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mali Asili na Utalii, Dk Allan Kijazi, alisema limeibuka wimbi jipya la ujangili wa tembo.

Alisema Tanapa wana mikakati ya kushusha ujangili wa tembo licha ya kuwa limeibuka wimbi jipya la ujangili huo. “Kuna hatari ya kuibuka wimbi jipya la ujangili wa tembo. Majangili wameanza kuwaaminisha watu kuwa maini na mafuta ya tembo yanasaidia kuponya kansa ya ini, kansa ya kizazi na vidonda vya tumbo.

 

“Watu wameanza kuweka sumu kwenye maboga na misumari katika njia (shoroba) wanazopita tembo ili kuwaua. Majangili wanachukua meno halafu wanawaachia watu maini na mafuta.

 

“Niwaambie Watanzania hakuna kitu kama hicho. Hakuna uthibitisho wowote wa kisayansi kwamba maini na mafuta ya tembo yanaponya kansa ya ini, kizazi wala vidonda vya tumbo. Hatutasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayejihusisha na ujangili. Wananchi wasidanganyike,” alisema Dk Kijazi.

UJANGILI WA KITOWEO   

Dk Kijazi anasema ujangili wa kitoweo wa wanyama kama swala, nyumbu katika baadhi ya maeneo imekuwa ni biashara hadi nje ya nchi.

 

“Wananchi wafuate taratibu rasmi zilizowekwa kama wanataka kitoweo cha wanyamapori. Uzuri hili suala limekuwa halali sasa baada ya mheshimiwa rais kutangaza ruksa kufungua mabucha ya nyama pori nchi nzima. Wananchi wafuate utaratibu na wafungue biashara yao rasmi kihalali,” anasema Dk Kijazi.

 

Faru mnyama adimu

Faru ni miongoni mwa wanyama adimu lakini wenye mvuto mkubwa wa utalii. Hawa wapo katika kundi la spishi maalum ambao wapo kwenye hatari ya kutoweka.

 

Hii nayo ni changamoto ya Tanapa katika utekelezaji wa lengo la kufikia mapato ya dola za Kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.

 

Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi wa Tanapa ambaye ni Mratibu wa Faru Taifa, Philbert Ngoti, anasema Tanapa inafanya jitihada kubwa katika kuwahifadhi wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka.

 

Faru ni wachache sana na ni ngumu kukutana nao porini. Hadi sasa Tanzania nzima kuna idadi ya Faru wapatao 190 tu na ili kuhakikisha wanaendelea kuwepo, Tanapa ina lengo la kuhakikisha wanafikisha idadi ya Faru 205 ifikapo mwaka 2023.

 

Sababu kubwa ya Faru kuadimika ni ujangili ambapo pembe zake zina thamani kubwa, hivyo majangili huwatafuta kwa lengo la kuchukua pembe zao.

Mgogoro kati ya binadamu na wanyama

Hii ni changamoto nyingine ambayo Tanapa wamekuwa wakiifanyia kazi, kuhakikisha migogoro kati ya binadamu na wanyamapori inapungua ifikapo mwaka 2025.

 

Mgogoro huu hutokana na wanyama kuvamia makazi ya binadamu wanaoishi karibu na hifadhini. Wanyama hao wakivamia makazi ya watu, hula mazao yao, kuharibu mashamba na kuua binadamu.

 

Takwimu za Tanapa zinabainisha kuwa, takriban watu 50 hufariki dunia kila mwaka kwa kuuawa na wanyamapori. Pia takwimu hizo zinaeleza kuwa takriban ekari 5,000 huvamiwa na wanyamapori kila mwaka.

 

Hii maana yake ni kwamba kuna shida kubwa katika uhusiano baina ya binadamu walio karibu na maeneo ya uhifadhi na wanyamapori.

 

Tanapa wamekuja na mpango kazi ambao pamoja na mambo mengine, wanakusudia kutoa elimu kubwa kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya uhifadhi ili wajue namna ya kufanya wanapovamiwa na wanyamapori.

Utalii wa ndani

 

Ili kufikia idadi ya watalii milioni 5, watalii wa ndani ya Tanzania pia wanatakiwa kuongezeka. Kumekuwa na uhaba wa utalii wa ndani kwa Watanzania wengi, kwa kuwa takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya utalii unaofanyika ni wa watalii kutoka nje ya nchi.

 

Bado watu wana dhana kuwa utalii ni jambo la gharama sana lakini Tanapa wameeleza kuwa bei za watalii wa ndani ni sawa na bure. Kuna hifadhi ambazo Mtanzania akienda analipia Sh 5,600 tu ya utalii, hoteli Sh 30,000 kwa siku, gharama ambazo kila Mtanzania anazimudu.

 

Tanapa wanaendelea kuwasisitiza Watanzania kujenga kasumba ya kutembelea mbuga zao za wanyama, huo ni mtoko bora sana, hata ukiwa na familia yako.

 

Uimara wa Tanapa

 

Taasisi ya Ulaya ya Utafiti wa Ubora wa Viwango (ESQR), hivi karibuni iliipatia Tanapa, Tuzo ya Dhahabu ya ubora wa utoaji huduma kati ya nchi 51 zilizochaguliwa kutoka nchi 39 duniani.

 

Hii inamaanisha kuwa Tanzania kuna huduma bora sana kwa watalii ambao watakuwa wakivutika kuja kufanya utalii nchini kutokana na ubora wa huduma, hii inaweza kuchangia katika kufikia malengo ya mapato ya dola bilioni 6 ifikapo 2025.

 

Uwanja wa Ndege wa Ruaha hivi karibuni nao ulichaguliwa kuwa uwanja namba moja Afrika na wa pili duniani kuwa wenye mandhari nzuri zaidi kuliko viwanja vingine vyote vilivyopo hifadhini. Hiki ni kivutio kingine cha kuwaonyesha watalii kwamba Tanzania kuna miondombinu mizuri na urahisi wa kuzifikia hifadhi.

 

Hifadhi ya Serengeti nayo hivi karibuni ilichaguliwa kuwa hifadhi bora kuliko zote Afrika. Hii nayo ni hoja ya kuhamasisha utalii Tanzania ili kufikia malengo.

 

 

Hitimisho

Wakati janga la corona ambalo lilirudisha nyuma sekta ya utalii likiendelea kupatiwa ufumbuzi duniani kote, jitihada zinazofanywa na Tanapa bila shaka zinaweza kufanya wafikie lengo la kuongeza mapato ya utalii nchini.

 

Lakini rai kwa Watanzania ni kudumisha utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi za taifa kwa kuwa kuna vivutio vingi vizuri na kuna faida kubwa katika afya ya saikolojia, ndiyo maana Wazungu wanatoka mbali sana kuja nchini kwa ajili ya utalii.

 

Utalii siyo suala la Wazungu pekee, ni mtoko muhimu sana ambao Mtanzania yeyote anaweza kufanya na familia yake na kufurahia Utanzania wake.

Na Mwandishi Wetu

Leave a Comment