
DAR: Uwanja wa mpira wa miguu wa Kirumba jijini Mwanza umegeuzwa danguro linalotumiwa na akina dada wanaojiuza nyakati za usiku maarufu kama ‘machangudoa’.
Uchunguzi uliofanywa na UWAZI jijini Mwanza umegundua kuwa eneo la nje la uwanja huo ambalo lima fremu za maduka ndipo hutumika na dada poa hao kufanyia uasherati kwa malipo maalum.
Baadhi na akina dada hao walipohojiwa na mwandishi wetu walikiri kufanya vitendo hivyo katika fremu za uwanja huo wanapopata wateja wanaume ambao hawana fedha za kuwapeleka kwenye nyumba za kulala wageni.
Akina dada hao walisema katika shughuli hiyo isiyo halali huwatoza wateja wao kati ya shilingi 5,000 hadi 7,000 kwa mara moja.
Walisema sehemu kubwa ya uwanja huo kwa nje nyakati za usiku huwa hauna taa hivyo giza hutanda na kurahisisha kazi yao.
“Mimi naitwa Frida, nafanya kazi hii kwa miaka 10 sasa na natunza familia. Ninapotoka usiku ndugu na majirani wanajua kuwa nakwenda kufanya kazi ya baa lakini ukweli ni kwamba najiuza,” alisema Frida.
Alisema kazi yao inafanywa na wanawake zaidi ya 50 eneo hilo na ili kuwa salama wana kijana wao ambaye huwa wanamlipa Sh.1000 kwa kila anayekwenda kutimiza haja zao kwenye fremu hizo za uwanja.
“Kijana huyu anatulinda sisi na wateja wetu ili wasitudhulumu. Unajua kuna wateja wengine wakorofi, hivyo kijana huyo huwa msaada kwetu kwa kuwa naye ni mtemi,” alisema Frida.
Alipotafutwa na UWAZI, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mwanza ambaye ndio wamiliki wa uwanja huo, Julius Peter alipoulizwa juu ya madai hayo alisema hana taarifa hizo za uwanja kugeuzwa danguro.
“Ngoja nifuatilie kwa kuwa mambo hayo hufanyika usiku kwa kificho. Kama ni kweli tutachukua hatua ili kulinda heshima ya chama na uwanja wenyewe,” alisema.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, ACP Muliro Jumanne Muliro alipoulizwa alisema hana taarifa japokuwa jambo hilo huwa gumu linapofikishwa mahakamani.
“Ili kukomesha biashara hiyo haramu inabidi kwanza wakamatwe wateja ambao ni wanaume. Hata hivyo, huwa hakuna ushahidi wa kutosha machangudoa wanapopelekwa mahakamani,” alisema.
HABARI; Elvan Stambuli, Uwazi