×

Jay Melody; ‘Mchawi’ wa Nandy!

UKIAMBIWA utaje wasanii waliotoka kwenye Jumba la Vipaji Tanzania (THT), lililokuwa likiasisiwa na marehemu Ruge Mutahaba, huwezi funga hesabu bila kutaja jina la kijana mwenye sauti ya aina yake Jay Melody.

 

Jina lake halisi anaitwa Sharif Said, ni mtoto wa mwisho kati ya familia yenye watoto watano.

Jay Melody ameanza kutambulika kwa mashabiki na ngoma ya Goroka ambayo imekuwa ikifanya vizuri mpaka sasa katika mitandao mbalimbali.

 

Vibao vingine ni kama, Cheche, Zeze, Mikogo Siyo, Namwaga Mboga na kwa sasa anatamba na ngoma yake ya Chini.

Ukiachilia mbali na kuimba, jamaa huyu pia ni mtunzi mzuri sana wa nyumbo, unaweza kumuita hata mchawi wa mastaa wengi sana Bongo.

 

Kwani asilimia kubwa ya wasanii huwa anawatungia nyimbo. Mfano mkubwa ni mwanadada Faustina Charles ‘Nandy’ karibia nyimbo zote anatungiwa na mkali huyu.

 

RISASI: Hongera kwa kazi nzuri unazoendelea kuzifanya kwenye muziki.

JAY MELODY: Ahsante sana.

RISASI: Tunaelekea kuumaliza mwaka sasa mipango yako iko vipi hasa kuzidi kulikuza jina lako?

 

JAY MELODY: Kikubwa ni kufanya kazi nzuri ambayo itapendwa na mashabiki zako, mwaka ujao naamini kwamba utakuwa ni mwaka wangu wa mabadiliko sitakamatika.

RISASI: Unaonaje ushindani uliopo kwenye muziki kwa sasa, utawezana kweli?

JAY MELODY: Kwa sasa ushindani umekuwa mkali kwa sababu muziki wa sasa umekuwa wa biashara ndiyo maana ubunifu umekuwa mwingi sana.

 

RISASI: Kwenye gemu hili unajiona na kitu gani cha kitofauti?

JAY MELODY: Napenda kufanya vitu vyangu mimi kama mimi ili kufika pale ambapo mashabiki zangu wanahitaji nifike, sipendi kufanya kitu eti kisa fulani anafanya hivyo.

 

RISASI: Unajiona nani kwa miaka ijayo…

JAY MELODY: Najiona msanii kubwa sana na ni ndoto yangu ya kila siku.

RISASI: Umekuwa na staili ya kuchelewesha kutoa nyimbo labda tatizo liko wapi?

 

JAY MELODY: Ni kweli, ila kwa sasa sitakuwa nachelewesha kutoa nyimbo kama ilivyokuwa hapo awali, nitawapa mashabiki zangu back to back (ngoma baada ngoma).

RISASI: Wasanii wengi wana ile ya kurudisha heshima kwa jamii kutoa misaada lakini kwako hatujaona ukifanya hivyo.

 

JAY MELODY: Hicho ni kitu kizuri sana, lakini siyo lazima tufanye kwa pamoja kila mtu ana wakati wake wa kufanya hayo.

RISASI: Wewe ni mmoja kati ya zao la THT labda unazungumziaje jumba hilo?

 

JAY MELODY: Ni sehemu ambayo nimeanza kufanya kazi yangu ya muziki, pale ni kama chuo cha kijifunza pia ninashukuru sana maana bila pale mimi nisingefika hapa nilipo.

RISASI: Una ngoma kali sana ambazo umezifanya labda mipango iko vipi kwenye kuzitengenezea EP au album?

JAY MELODY: Mipango iko sawa kabisa hata mimi natamani sana nifanye hivyo ila kwa sasa nasoma kwanza soko liko vipi.

 

RISASI: Wewe ni mtunzi mzuri sana wa nyimbo labda unajivunia nini katika hilo.

JAY MELODY: Unajua kuwa mtunzi ni kipaji kingine pia, kwa mimi nilikuwa nadhani najua tu kuimba kumbe hata kutunga nyimbo naweza, kiukweli nina furaha sana kwa hiki kipaji nilichokuwa nacho.

 

Na pia ninakifanyia kazi ili kuhakikisha hakipotei kwa sababu nusu ya maisha yangu kwenye muziki ni uandishi, mara nyingi napata pesa kwenye kuandikia wasanii nyimbo.

RISASI: Ni wasanii gani ambao umewahi kuwatungia nyimbo na zikafanya vizuri?

 

JAY MELODY: Nimewatungia wasanii wengi sana, Nandy nimemtungia nyimbo nyingi.

RISASI: Hizo nyimbo unazowatungia ni kiasi gani cha fedha wanakulipa?

JAY MELODY: Inategemea kwa sababu siyo kila msanii unayemuandikia anakulipa, wengine unakuta hana pesa kabisa na ni rafiki yako lazima umsaidie pengine na yeye atakuja kukusaidia.

 

RISASI: Mipango yako ipo vipi kwenye kufanya kazi nyingi zaidi.

JAY MELODY: Ni kufanya kolabo nyingi zaidi, lakini pia natamani kufikisha muziki wangu kimataifa zaidi, kingine natamani sana kuwa msanii mwenye mafanikio unajua wasanii wengi wanafanya kazi sana ila hawana mafanikio.

RISASI: Ni msanii gani hapa Bongo unamtazama kama role model wako?

 

JAY MELODY: Kwa mimi nawapenda wasanii wote, nikimuona msanii yeyote anayefanya vizuri kwangu anakuwa kama kivutio na kutamani kuwa kama yeye, nikisema mmoja itakuwa siwatendei haki wengine.

RISASI: Tukirudi kwenye upande wa familia vipi kuhusiana na mke na watoto?

 

JAY MELODY: Bado sijabaatika kupata mke wala mtoto.

RISASI: Mashabiki wangependa kufahamu Jay Melody ni mtu wa aina gani.

JAY MELODY: Ni mtu wa kawaida sana, mpole mstarabu, pia ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto 5, Jay Melody siyo jina langu kamili mimi naitwa Sharif Said.

MAKALA | KHADIJA BAKARI

Leave a Comment