
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar-es-saalam, imewasomea maelezo ya awali wanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) wakiwemo wabunge wa viti maalum, Halima Mdee, Esta Bulaya na Esta Kishoa.
Watuhumiwa hao ni, Halima Mdee, Ester Bulaya Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa, Boniface Jacob, Henry Kilewo, yohana Kaunya ,Patrick Assenga, Kedmony Mhembo, Mshewa Karua, Athumani Hassani na Gerva Yende.
Wengine ni, Angela Tryphone, Khadija Mwango, Reginald Masawe , Pendo Raphael, Cesilia Michael, Happy Abdallah, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Hamis Yusuph,Steven Ezekiel, Juma Hussein, Mustafa Lada Emanuel Zakaria na Paulo Makali.
Washitakiwa hao wamesomewa maelezo ya awali na wakili wa Serikali Mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude, sambamba na wakili wa Serikali Faraji Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi.
Kabla ya kuwasomea maelezo ya awali, wakili Mshanga aliwakumbusha Mashitaka yanayowakabili washitakiwa.
Ambapo amedai Machi 13, mwaka 2020 washitakiwa wote wakiwa katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, isivyo halali na kwa makusudi walikaidi amri iliyotolewa na askari B 3648 SGT John ambaye aliwataka wahusika hao kuondoka eneo hilo la magereza na alikuwa akitimiza wajibu wake aliyopewa.
Katika shtaka la pili, kufanya mkusanyiko usio halali, Inadaiwa Machi 13, 2020 katika eneo la gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam washitakiwa wote kwa pamoja walikusanyika katika eneo hilo la magereza isivyo halali hali iliyopelekea kuleta hofu na kuhatarisha amani na utulivu kwenye eneo hilo.
Katika shtaka la tatu,kuharibu mali, alidai kuwa Machi 13, mwaka 2020 eneo la gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala washitakiwa hao wote kwa pamoja walishirikiana kufanya uharibifu wa geti la Segerea ambalo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia inadaiwa Machi 13, mwaka 2020 katika gereza la Segerea mshitakiwa Mdee alitoa maneno ya kuudhi kwa askari magereza Sajent John, maneno ambayo yalipelekea uvunjifu wa amani.
Katika mashitaka ya kutoa lugha ya kuudhi ambalo linamkabili Bulaya, inadaiwa Machi 13, mwaka 2020 mshitakiwa huyo akiwa maeneo ya gereza la Segerea alitoa maneno ya kuudhi kwa Sajenti B 3648 John na kusababisha uvunjifu wa amani.
Mshitakiwa Jacob anadaiwa Machi 13, mwaka 2020 akiwa eneo la gereza la Segerea alitamka maneno ya kuudhi kwa Sajenti B 3648 John pamoja na kufanya shambulio kwa askari magereza kwa kumkunja na kumvuta shati askari huyo wakati akitekeleza majukumu yake.
Baada ya kuwakumbusha Mashtaka wanayokabiliwa nayo upande wa Jamhuri umewasomea hoja za awali zikiwa ni pamoja na majina yao, chama wanachotokea na maelezo yote ya Mashtaka wanayokabiliwa nayo.
Washitakiwa wote kwa pamoja walikubali maelezo ya majina yao,sambamba na kuwa ni wanachama wa Chadema na kukana maelekezo ya Mashtaka yao, lakini mshitakiwa namba nane (Edga Adeline) na mshitakiwa namba 15 (Reginald Masawe) wao hawakufika Mahakamani kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.
Washitakiwa hao wanaendelea kuwepo nje kwa dhamana hadi Mei, 15 mwaka huu ambapo mashaidi 22 wanategemewa.