
WINGA mpya wa Yanga, Dickson Ambundo amefunguka kuwa yuko tayari kupambana ili kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza licha ya upinzani atakaokutana nao kutoka kwa Mkongomani Jesus Moloko na Farid Mussa.
Ambundo amejiunga na Yanga katika dirisha hili la usajili akitokea klabu ya Dodoma Jiji baada ya kuwa na wakati mzuri msimu uliopita, akihusika kwenye mabao 11 ambapo alifunga mabao manne na kuasisti mara saba kwenye michuano yote.
Kwenye mchezo wa Jumapili iliyopita dhidi ya Zanaco, Ambundo aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Farid Mussa ambapo licha ya kucheza dakika chache alifanikiwa kuonyesha uwezo mzuri.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ambundo alisema: “Nilijiunga na Yanga nikijua wazi kuna changamoto ya namba kwa sababu hii ni timu kubwa, lakini kama mchezaji mwenye malengo ya kufika mbali hiyo haiwezi kuwa tatizo bali itanisaidia kujituma na kukua zaidi.
“Hivyo nipo tayari kupambana na nitahakikisha ninafanya kila jitihada kuonyesha uwezo wangu, ili kumshawishi kocha aniamini na kunipa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza,” alisema staa huyo.
Tangu ajiunge na Yanga Ambundo amefanikiwa kuhusika kwenye bao moja kufuatia asisti yake kwenye mchezo dhidi ya Nyasa Big Bullets, kwenye michuano ya Kombe la CECAFA Kagame iliyofanyika Dar es Salaam mwezi Agosti.
STORI NA JOEL THOMAS, CHAMPIONI IJUMAA