×

Lingard Ajutia Kosa Lake Lililoigharimu United

JESSE Lingard amekiri kuwa ameumizwa baada ya kosa lake kusababisha Manchester United kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu dhidi ya Young Boys, juzi Jumanne.

Kiungo huyo wa Man United alicheza pasi ya hovyo ya nyuma kwa kipa David de Gea iliyodakwa na Jordan Siebatcheu aliyefunga bao la ushindi dakika ya 95 kwa kikosi hicho cha nchini Uswisi.

Lingard alikuwa ameingia dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Cristiano Ronaldo, na ingawa nyota huyo, 28, amechukizwa na kosa hilo la dakika ya mwisho, amesisitiza watu wasisahau kuwa makosa hutokea kwenye mpira.

“Inauma sana,” aliandika kwenye Twitter. “Kila ninapovaa jezi, natumaini watu wanaelewa inamaanisha nini kwangu.

“Daima nataka kwenda kufanya kilicho bora kwa ajili ya klabu, timu na mashabiki. Nimevurugwa na nilivyochangia kipigo. Makosa hutokea kwenye mpira lakini tunajiinua na kwenda tena.”

MANCHESTER, England

Leave a Comment