Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo na tayari kuna kila dalili ya siri kufichuka.
Grace na Magesa wakiwa wanaendelea na mazungumzo, mwanamke huyo jasusi anagundua kitu kuhusu laptop ya Magesa na sasa anajitahidi kufanya kitu ili kutunza taarifa za siri zilizokuwa ndani ya laptop hiyo.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Akamuonesha laptop ndogo ambayo juu yake kulikuwa na ramani ya mtandaoni ikionesha kilichokuwa kinafanyika ndani ya laptop hiyo. Magesa akabaki amepigwa na butwaa, kwanza alishangaa iweje Grace awe na uwezo wa kujua kitu kama hicho na pili ni akina nani waliokuwa wakishughulika na laptop yake.
“Ina siri nyingi sana ndani yake, hata sijui itakuwaje,” alisema Magesa lakini Grace akamwambia asiwe na wasiwasi kila kitu kitakuwa sawa.
“Kwenye laptop yako uliwahi kuweka programu yoyote ya Encycription?”
“Ndiyo kitu gani hicho?” alihoji Magesa huku akionekana kutoelewa kilichokuwa kinazungumzwa na Grace.
“Encycription ni mbinu ya kiteknolojia ya kubadilisha taarifa zako (data) kwenda katika mfumo ambao mtu mwingine hawezi kuelewa kwa urahisi. Ndiyo maana nilitaka kujua kama uliwahi kuweka programu kama hiyo kwenye laptop yako.”
“Mh! Hapana, kusema kweli sijawahi kwa sababu hata sikuwa najua ni kitu gani na kina umuhimu gani.”
“Niliwahi kukuingizia programu inaitwa CryptoForge bila wewe mwenyewe kujua chochote ila sijui kama inaweza kuwa inafanya kazi mpaka leo, ngoja nijaribu,” alisema Grace na kumfanya Magesa akose cha kujibu. Hakuna jambo lililomfanya ajione hana akili kama kitendo cha laptop yake kufuatiliwa kwa karibu na Grace kwa kipindi kirefu wakati mwenyewe akiwa hajui chochote.
“Kuna haja ya kwenda kusomea mambo ya teknolojia ya mawasiliano ili na mimi niende sambamba na kasi ya dunia kuwa kijiji,” aliwaza Magesa wakati akimtazama Grace alivyokuwa anaonesha uwezo mkubwa wa kutumia mitambo iliyounganishwa na kompyuta.
* * *
Kwa kutumia teknolojia za kisasa za Power ISO na Password Cracker, Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa na vijana wake, walifanikiwa kuifungua laptop ya ‘marehemu’ Magesa na kuanza kufuatilia mawasiliano ya barua pepe kati ya Magesa na Mwampashi enzi za uhai wao.
“What is going on!” (Nini kinaendelea?) Mandiba alihoji baada ya kuhisi kuna kitu kisichokuwa cha kawaida kilikuwa kikiendelea kwenye ile laptop, wale vijana wote wakaacha kila walichokuwa wanakifanya na kuisogelea laptop hiyo ambapo katika hali ambayo hakuna aliyeelewa imesababishwa na nini, iligoma kufanya kazi huku ikianza kupata joto la ajabu.
Kufumba na kufumbua, vitu vyote vilivyokuwa ndani ya laptop hiyo, kuanzia nyaraka, picha na sauti zilibadilika ghafla na kuwa kwenye mfumo usioeleweka, maandishi yakiwa yamebebana na kuchanganyikana na namba na alama nyingine za ajabu.
“What is this?” (Hiki ni nini)
“We have been hacked! All the data has been translated into secret codes, it seems someone is behind this! (Tumefanyiwa udukuzi! Taarifa zote zimebadilishwa kwenda kwenye lugha ya siri, inaonesha kuna mtu nyuma ya hili jambo.)
“Cant we revert the changes? All data must be recovered, its very important (hatuwezi kubadilisha na kurudisha kila kitu kama ilivyokuwa mwanzo? Taarifa zote lazima ziokolewe, ni muhimu sana) alihoji Mandiba huku akionesha kuchanganyikiwa kwa sababu kama hilo lingeshindikana, maana yake wangekuwa wamefanya kazi bure na kukwama hatua za mwisho kabisa.
Waliendelea kuhangaika kwa muda mrefu huku wakijaribu pia kufuatilia ni nani aliyewafanyia kitendo hicho kwa sababu walikuwa na imani kubwa kwamba walikuwa wakifanya kazi kwa usiri mkubwa.
Wakati wakiendelea kuhangaika huku na kule, Mandiba aliwapigia simu vijana wake wengine waliotumwa kuifuatilia laptop ya Mwampashi ambapo GPS (Global Positioning Sysytem) ilikuwa inaonesha kwamba ipo Mwenge.
“That is the only chance which we have right now! Don’t mess up you guys!” (Hiyo ndiyo nafasi pekee tuliyonayo kwa sasa, msije mkafanya uzembe vijana) alisema Mandiba kwa msisitizo wakati akizungumza na vijana wake hao kwa simu.
* * *
“Kwisha kazi.”
“Unamaanisha nini Grace.”
“Hawataweza kuona chochote ndani ya laptop yako, nimevuruga kila kitu,” alisema Grace huku akiinuka na kwenda kumkumbatia Magesa kwa mahaba, wakabusiana huku Magesa akishusha pumzi ndefu baada ya kuhakikishiwa usalama wa taarifa zake.
“Lakini unafikiri ni nani anayeweza kuwa anafanya mchezo huo?”
“Hata sijui lakini inaonesha kuna watu wanaendelea kunifuatilia. Kwa nini waende kuchukua laptop nyumbani kwangu?”
“Hata kama wanakufuatilia haitakuwa rahisi kufahamu jambo lolote, niamini mimi,” alisema Grace, wakakumbatiana huku mwanamke huyo akimbusu Magesa kimahaba.
“Hatutakuwa na muda wa kuendelea kukaa sana hapa, kuna sehemu nyingine tutakwenda, mbali kabisa na hapa,” alisema Grace.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.