Ilipoishia wiki iliyopita
Nesi huyo akashika kidude kinachoendesha kompyuta iliyokuwa mbele yake, akabonyeza bonyeza vitufe kadhaa na akaelekeza macho yake kwa umakini kusoma kilichoandikwa ndani.Sasa endelea…
Akatazama vizuri zaidi na macho yake yalionyesha kama kuna kitu alikibaini, maana yalionyesha mabadiliko ambayo yeyote angeweza kuhisi kitu.
“Kwani hawa wagonjwa ni nani zako,” yule nesi alimuuliza Bata, ambaye sura yake bado ilionyesha hofu ya kutojua nini kinaendelea.
“Ni walezi wangu,” alijibu Bata kwa kujiamini.
“Pole sana, bahati mbaya wote wamefariki, ajali ilikuwa ni mbaya mno, maiti zao zimepelekwa chumba cha kuhifadhia maiti, kama utawahitaji wasiliana na ndugu zako muende mochwari,” alisema nesi huyo huku akimtazama kwa masikitiko kijana aliyekuwa mbele yake.
Bata alitegemea kauli hiyo, maana kwa muda wote mwili wake ulikuwa unatetemeka tu. Lakini hata hivyo baada ya kuelezwa suala hilo, kitu kama mshale wa moto ukapita katikati ya mwili wake, akajisikia kupoteza nguvu ya mwili na kiakili. Akakaa chini kwa sekunde chache, kisha akainuka na kutoka nje ya wodi.
Akatoka nje ya hospitali, akaingia katika mtaa asioujua, akaendelea mbele, akavuka barabara akaendelea mbele, akikatiza mtaa mmoja baada ya mwingine hadi alipojisikia njaa ikimuuma. Alikuwa na hela amebaki nayo mfukoni, akasogea kwa mama ntilie mmoja, alipouliza chakula, akaambiwa umebakia ukoko tu, atauziwa kwa shilingi mia tano, akaomba apewe!
Baada ya kumaliza kula, akaendelea kuzunguka katika mitaa ya Kariakoo. Hakuwahi kufika hata siku moja, hakuelewa apite wapi ili atokezee wapi, kwa vile hakujua aende wapi. Jua lilipoanza kuzama, ndipo akili ikamjia na kumfahamisha kuwa alipaswa kujua sehemu ya kulala.
Hadi saa tatu za usiku, alikuwa bado anazunguka katika mitaa hiyo na baadhi ya barabara zikaanza kupungua watu. Katika jengo moja, akawaona watu wamekaa kwenye kingo za kuta, wakubwa kwa wadogo, naye akatafuta eneo akaenda na kukaa, akiegemea ukutani.
Hata alipopitiwa na usingizi hakujua hadi mbu waliokuwa wakimuua kwa bidii walipomuamsha usiku wa manane. Alipofumbua macho, akakuta watu wengine zaidi wamelala kando yake. Kuona hivyo, akapata amani, naye akajichomeka katikati yao vizuri na kulala hadi kulipokucha.
Mmoja wa waliolala naye, alimuuliza kazi anayofanya mchana, lakini Bata hakuwa na cha kufanya, akamueleza ukweli kijana huyo ambaye alionekana kidogo mkubwa kuliko yeye. Akamweleza amfuate, akaongozana naye hadi shimoni, sokoni Kariakoo.
Akamwelekeza jinsi ya kufanya. Wakiokota viazi, nyanya, vitunguu na mazao mengine ya kilimo yanayodondoka kwenye magunia yanayopakuliwa kwenye malori. Baada ya kukusanya, walitoka nje ya soko kiasi cha saa tatu asubuhi na kupanga mafungu nje ambako waliuza na hivyo kujipatia kipato chao cha kila siku.
Hayo ndiyo yakawa maisha mapya ya Bata ambaye hata hivyo, wenzake wakamwita Chongo, kutokana na jicho lake moja kutokuwepo. Kuanzia wakati huo, jina lake likapotea, akajulikana zaidi kwa jina hilo jipya.
Miaka miwili ya kuokota mazao ya kilimo pale sokoni Kariakoo, ikamfanya kijana huyo kujulikana karibu soko zima. Na kilichompa umaarufu zaidi, ni bidii yake kazini, kwani aliachana na kuokota badala yake, akajiwekea fedha hadi akaweza kununua bidhaa hizo kutoka kwa wauzaji wa jumla.
Akawa na meza yake na maisha yake yakabadilika kidogokidogo, kwani aliacha kulala katika vibambaza vya nyumba za watu, akapanga chumba huko uswahilini Manzese.
Alipofikisha umri wa miaka kumi na nne, tayari alishakuwa na uzoefu wa biashara, kwani aliacha kuuza genge, akajihusisha na mitumba, akinunua nguo zinapokatwa, kisha yeye kutembeza mitaani na kwenye maofisi.
Na cha kufurahisha zaidi, Chongo akawa mtu wa kujipenda, akivaa vizuri na akanunua miwani miyeusi, iliyoficha uso wake hivyo watu wengi wageni kwake wakawa hawajui kama alikuwa na tatizo la macho!
Siku moja, baada ya zaidi ya miaka saba tangu aanze kujishughulisha, akiwa amewasahau watu wake wote wa karibu, alikuwa ameweka viatu vyake vya kiume na kike katika kibaraza cha jengo moja kubwa lililoko mtaa wa Samora, nyakati za mchana, wafanyakazi wakienda kula.
Mara akatokea mtu akija kwa mwendo wa polepole, akionekana kama ambaye siyo mgeni maeneo hayo, akamkazia sana macho. Alikuwa anamkumbuka, lakini alichosahau ni lini na wapi alimuona.
Mtu huyo akampita na mbele kidogo akaingia ndani ya jengo hilo lenye ghorofa kumi. Alimtazama hadi alipoingia ndani ya lifti na kupanda juu, akimuacha Chongo akiwa ametahayari!
Je, ni nani ameonekana machoni mwa Chongo? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo!