
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Shinyanga imemhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha nje miezi sita mwanafunzi Kunde Gambija (16) ambaye alifanya mtihani wake wa kuhitimu Elimu yake Msingi akiwa ndani ya gereza la Wilaya ya Bariadi huku Baba yake Gisabu Sayi Mahila akifungwa kifungo cha Miaka mitano gerezani.
Mwanafunzi huyo pamoja na Baba yake walikuwa wakikabiliwa na kesi ya jinai namba 66 ya mwaka 2021 ya kuua bila ya kukusudia katika mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga.
Awali Kunde Gambija pamoja na Baba yake Gisabu Mahila walikabiliwa na kesi ya mauaji kabla ya hati mashtaka kubadilishwa na kuwa kesi ya kuua bila ya kukusudia kutokana na mazingira ya tukio lilivyotokea.
Walidaiwa kumuua Gegedi Kulabya (57) kinyume na kifungu cha 195 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, tukio ambalo walilitenda Julai 7,2021 majira ya saa 5 usiku uko nyumbani kwao katika kijiji cha Dasina kata ya Nkoma Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Na Derick Milton | GPL