×

Ndoa na Shetani-2

ILIPOISHIA:
“Mavazi gani hayo, yaani umbile kama lako ningekuwa nalo mimi kila mtu angenisoma namba. Mungu amekupendelea ili uutangaze uwezo wake wa uumbaji ukilificha, usije shangaa siku moja ukasikia umekuwa mlemavu kwa kushindwa kuvitangaza..kwanza unajijua wewe mzuri?” niliuliza huku akinitazama.

“Nitajijuaje mwenyewe?”
“Ina maana kote ulikosoma hukuwahi kusifiwa?”
SASA ENDELEA…

“Hiyo hali nimeshaizoea.”
“Basi Konso wewe ni mzuri chuo kizima, yaani ningekuwa kama wewe mbona wangenikoma!”

Suzy alikuwa msichana mjanja kuliko mimi, starehe kwake kilikuwa kitu cha kawaida eti hata wazazi wake walilijua hilo kwa kumuachia kujirusha, la muhimu akili yake ilikuwa ikichaji.

Ushawishi wa Suzy haukuwa mkubwa kwa sababu hata mimi starehe nilikuwa nazipenda, lakini ndiyo hivyo ni nilikuwa kwenye geti kali. Kwa kweli nilijikuta naungana na Suzy kwenda kwenye kumbi za starehe usiku. Huku nako Suzy alikuwa na rafiki yake wa kiume na mimi alinitafutia rafiki yangu.

Mabwana tuliowapata walikuwa na pesa za kumwaga, ilifikia hatua ya kusafiri nje ya mkoa kwenda kwenye miji ya starehe. Ajabu bwana wa Suzy alifanya mapinduzi kwa kunitangazia dau kubwa kwa kuwa mimi nilikuwa mzuri kuliko Suzy. Kibaya niliyekuwa natembea naye ni rafiki yake na pesa alikuwa akitoa yeye.

Yule bwana alisababisha mimi na shoga yangu tuwe maadui wakubwa tukawa chui na paka, hata kufikia hatua ya kutengana chumba na kununiana. Hatukuwa tukiongea, ulikuwa uhasama mkubwa na kutishiana kuuana.

Yule bwana aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Moses au kama alivyokuwa akipenda kujiita ‘Emma Mo’. Aliamua kunihamisha shule na kunipangishia Uswahilini lakini sehemu ya watu wenye uwezo.

Aliniwekea kila kitu muhimu ndani, nilijikuta nasahau maisha ya chuo na kuishi maisha ya starehe ya kila mwisho wa wiki, lazima tutoke kwenda kwenye kumbi za starehe. Emma Mo aliniambia niache kusoma kwa kuwa anataka kunioa na kunipa maisha mazuri.

Nilikubali kuacha shule bila wazazi wangu kujua, niliamua liwalo na liwe hata kama wakijua watasema watakachoka na mwisho watalala. Emma Mo alikuwa tayari kuwalipa kiasi chochote cha gharama ya masomo yangu kuanzia chekechea.

Niliishi na Emma Mo kwa mwaka mmoja nikiwa sijui kupika wala kufua. Niliishi kama malkia na yeye aliniita malkia wake, kwa kweli kila sehemu tuliyokwenda walimuuliza amenitoa wapi malaika ambaye hawaamini nilizaliwa bali nimeshushwa kwa uzi wa buibui.

Na sehemu zote nilikuwa nakwenda naye katika mavazi ya ajabu ya nusu utupu, nilipomgomea alisema kama Suzy:

“Lazima niutangaze utaalamu wa Mungu kwa utundu alioufanya kukuumba, nina imani siku aliyokuumba aliacha shughuli zote na kukuumba kwa umahiri wa hali ya juu.”
Mwanzo nilikuwa naona kazi lakini nilikuja kuyazoea na kuona kutembea uchi au nusu uchi ni jambo la kawaida tu. Pamoja na kuwa na pesa nyingi lakini nilikuwa sijui kazi ya Emma Mo. Alikuwa mwanaume mwenye pesa, alizichezea kama anazitengeneza mwenyewe. Tena alipokuwa akisafiri na kurudi, alirudi na fedha nyingi ambazo zilikaribia kujaa kwenye kabati.

Nilijiona mwanamke mwenye bahati, Mungu kanijalia umbile zuri pia kupata mwanaume mwenye fedha. Maisha niliyoishi na Emma Mo sikuwahi kuyaota hata ndotoni. Hakuna kitu nilichokitaka nikakikosa, tulisafiri nchi za nje kula starehe.
Maisha yaliendelea, nakumbuka siku moja tukiwa tumelala majira ya saa saba usiku nyumba yetu ilivamiwa na maaskari.

Emma Mo pamoja na mimi tulichukuliwa juujuu na kupelekwa polisi usiku huo huo. Kwa upande wangu sikujua tumechukuliwa kwa sababu gani.
Kabla ya kutuchukua walifanya upekuzi mzito kitu kilichonishangaza na kujiuliza kulikuwa na nini!

. Tulipofika polisi tulitenganishwa kila mmoja aliwekwa sehemu yake, tulilala pale pale hadi asubuhi. Kesho yake majira ya saa saa tano tulitolewa kwa dhamana na rafiki zake Emma Mo, walikuwa ni watu wenye pesa sana.

Mpaka tunarudi nyumbani sikujua jana yake tulichukuliwa na polisi kwa kosa gani, kila nilipomuuliza alinijibu kwa mkato “Achana nayo.” Pamoja na kukaa kimya bado nilikuwa kwenye maswali mazito juu ya kuvamiwa na polisi wenye bunduki nzito na mbwa kama jambazi au mhaini.
****
Jioni ya siku ile Emma Mo alinieleza kuwa tatizo lake ni zito kwa hiyo anatakiwa kuondoka nchini usiku ule. Nilijiuliza ni tatizo gani linalomkimbiza nchi.
“Sasa utarudi lini?” nilimuuliza.

“Kwa kweli haijulikana ikiwezekana kuonana majaliwa.”
“Oooh Mungu wangu, na mimi itakuwaje?”
“Sina jinsi itanibidi nikuache kwa sababu tatizo lenyewe limetokea ghafla.”
“Mimi nitaishi vipi kwa kuwa wewe ndiye umeniachisha shule?” nilimuuliza nikiwa nimetaharuki.

“Siwezi kukuacha kwenye hali mbaya bali nitakuachia pesa nyingi, nina imani itakutosha kununua nyumba na gari zote nimekuachia.”
“Kiasi gani cha fedha unaniachia?”

“Milioni 70 ila ndani ya nyumba hii unatakiwa kuanzia kesho uondoke nyumba si mali yetu tena, nimeiuza ili kupata nauli na pesa ya kukuachia.”

Nilitamani kulia kwa kujua sasa ndipo wakati wa kuadhirika mtoto wa kike kwa sababu Emma Mo alikuwa amenizoesha vibaya sana. Sikuwa na jinsi nilimuagia pale pale kwa sharti hatakiwi kusindikizwa na mtu. Baada ya Emma Mo kuondoka nilirudi kwenye chumba.

Baada ya kuondoka sikuona sababu ya kulia au kuhudhunika sana kwani Emma Mo alikuwa kaishanifungulia maisha nilitakiwa kuyaendeleza. Nilijikuta nikiwa njia panda nifanye nini na zile pesa. Wazo la awali lilikuwa kurudi nyumbani na kuomba msamaha kwa wazazi wangu.

Lakini nilijiuliza nitawaeleza nini ili wanielewa ikiwa nimewatia hasara kubwa. Niliamua maisha yangu yawe mbele kwa mbele sikutaka kurudi nyuma. Kama pesa nilikuwa nayo ya kuishi maisha yoyote ninayotaka. Nilisimama mbele ya kioo kuthibitisha uzuri wangu. Uzuri wangu ulikuwa umeongezeka maradufu, kioo kilinilithibitishia mimi mzuri tena sana.

Nilikuwa nikiona fahari kusimama kwenye kioo kwa muda mrefu kwa kuuangalia uzuri wangu. Baada ya kununua nyumba na kuuza baadhi ya magari nilianza maisha mapya ya kujitegemea, bado niliishi maisha ya kifahari ya kujirusha kila kumbi ya starehe sikukosa mwisho wa wiki.

Siku zote kizuri chajiuza, nilichukua muda wa miezi mitatu toka Emma Mo kuondoka kupata bwana mwingine. Nilimpata kijana wa Kiarabu ambaye nilimchanganya na kutangaza ndoa.

Kwa kweli ilikuwa harusi kubwa sana ambayo nina imani mpaka Mungu ananichukua haitatokea katika maisha yangu. Bwana huyu pesa alikuwa nayo, alikuwa akimiliki magari na vituo zaidi ya kumi vya mafuta jijini.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia katika Risasi Jumamosi siku ya Jumamosi.

Itaendelea Risasi Jumamosi

Leave a Comment