×

Unending Love – 66

ILIPOISHIA:
Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo.

Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inapozidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake kwa mara nyingine kwa madai kwamba anajihisi anakaribia kufa hivyo ni lazima aonane na Jafet ili amueleze kilichokuwa ndani ya moyo wake.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Jafet amebaki Tanzania Anna, si tulishazungumza kwamba kwa sababu mwenzako yupo chuoni na amekaribia kufanya mitihani abaki?” baba yake Anna alizungumza kwa upole na binti yake huyo.

“Baba, nahisi kama maisha yangu yanaelekea ukingoni, nilikuwa nahitaji kuzungumza na Jafet kabla sijafa,” alisema Anna, kauli iliyowafanya wazazi wake watazamane wakiwa ni kama hawaamini walichokisikia.

“Anna! Anna! Usiseme hivyo mwanangu, bado tunakuhitaji na tunaahidi kwamba tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha unapona,” alisema mama yake Anna huku akitokwa na machozi mengi.

Hali aliyokuwa nayo binti yake, ilimfanya taa nyekundu iwake kwenye kichwa chake, akamuinamia pale kitandani na kumkumbatia huku machozi mengi yakiendelea kumtoka. Baba yake Anna akawa na kazi ya ziada ya kuwabembeleza wote wawili kwani Anna naye alikuwa akilia uchungu.

“Hebu njoo tena nje tuzungumze mke wangu,” alisema baba yake Anna huku akimshika mkewe mkono, wakatoka hadi nje na kuanza kujadiliana nini cha kufanya. Mwisho wakakubaliana kwamba inabidi baba yake Anna asafiri haraka kurudi nchini Tanzania kwa ajili ya kwenda kumshawishi Jafet kama anaweza kukubali kusafiri mpaka nchini India kwa ajili ya kwenda kuonana na Anna ambaye kiukweli alikuwa kwenye hali mbaya kiafya.

Baada ya kukubaliana, walirudi wodini na baba yake Anna akamhakikishia binti yake kwamba anafunga safari kurudi nchini Tanzania kwa ajili ya kwenda kumchukua Jafet, taarifa iliyopokelewa kwa furaha na Anna, baba yake akamuinamia pale chini na kumbusu, naye akafanya hivyo huku tabasamu hafifu likianza kuchanua kwenye uso wake.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, kwa kuwa fedha hazikuwa tatizo kwa familia hiyo, baba yake Anna alifanya mipango ya kusafiri siku hiyohiyo na kwa bahati nzuri, alifanikiwa kupata nafasi kwenye ndege ya Fly Emirates waliyokuja nayo.

Hatimaye aliondoka na kumuacha Anna mikononi mwa mama yake, akimsisitiza kuhakikisha taratibu zote za matibabu, ikiwemo tiba mpya ya dialysis inafanyika kikamilifu. Kwa kuwa baba yake Anna aliondoka usiku nchini India, baada ya saa nyingi za kuwa angani, hatimaye aliwasili jijini Dar es Salaam alfajiri ya siku iliyokuwa inafuatia.

Baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alikodi teksi iliyompeleka moja kwa moja mpaka Chuo cha Udaktari na Tiba Shirikishi cha Muhimbili (MUCHS), alikokuwa anasoma Jafet.

Wakati ofisi zinafunguliwa asubuhi hiyo, tayari baba yake Anna alikuwa amewasili, akazungumza na mmoja wa viongozi wa chuo hicho na muda mfupi baadaye, Jafet akaenda kuitwa kwenye hosteli aliyokuwa anaishi.

Japokuwa alikuwa bado hajamaliza kujiandaa, Jafet alipoambiwa kuna mgeni wake asubuhi hiyo, alihisi kuna tatizo kubwa, bila kupoteza muda akatoka na kwenda kuonana naye.

Kitendo cha kumuona baba yake Anna asubuhi yote hiyo, huku uso wake ukionesha uchovu wa waziwazi, kilimshtua mno Jafet, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kwani alihisi ameletewa taarifa mbaya kuhusu Anna.

Mzee huyo akamshika mkono na kusogea naye pembeni, Jafet akawa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ataambiwa nini. Walisogea mpaka sehemu walipokaa siku ya kwanza, baba yake Anna akaanza kumueleza Jafet kila kitu kilichotokea.

Japokuwa kijana huyo alishaamua kusonga mbele kwenye maisha yake kwa kuwa na msichana mwingine, Suleikha, taarifa alizoletewa na baba yake Anna zilimfanya ajisikie vibaya sana ndani ya moyo wake mpaka mwenyewe akawa anajishangaa.

“Najua tunakusumbua sana lakini tuko chini ya miguu yako, uhai wa Anna uko mikononi mwako, tafadhali sana,” alisema baba yake Anna, Jafet akakosa cha kujibu kwa muda huo.

“Mimi sina tatizo ila inabidi nipate ruhusa kutoka hapa chuoni na kutoka kwa wazazi wangu,” alisema Jafet, wazo ambalo baba yake Anna hakulipinga. Kwa kuanzia, aliinuka na kuelekea kwenye ofisi ya Dean of Students (Mlezi wa Wanachuo) ambapo alienda kumuombea Jafet ruhusa na kueleza hali halisi ya dhumuni la ruhusa hiyo.

Baada ya kukubaliwa chuoni hapo, baba yake Anna alimuomba Jafet waongozane mpaka kijijini kwao, Rwamgasa huku akiahidi kugharamia kila kitu yeye mwenyewe. Bila hata kumuaga Suleikha, Jafet aliongozana na baba yake Anna mpaka Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere walikofanya taratibu zote muhimu na kufanikiwa kupata ndege iliyokuwa inaondoka asubuhi hiyo kuelekea jijini Mwanza.

Saa mbili baadaye, tayari Jafet na baba yake Anna walikuwa wameshawasili jijini Mwanza, wakaenda mpaka stendi kuu ya mabasi na kupanda basi lililokuwa lililowapeleka mpaka njiapanda ya Rwemgasa, wakateremka na kupanda usafiri mwingine wa pick-up na baadaye kuunganisha kwa usafiri wa baiskeli.

Saa tano za asubuhi, Jafet na baba yake Anna walikuwa wamewasili nyumbani kwa kijana huyo, kwa bahati nzuri waliwakuta wazazi wote wa Jafet nyumbani ambapo walipigwa na butwaa kumuona kijana wao akiwa ameongozana na baba yake Anna ambaye kwa kiasi kikubwa, kwa kushirikiana na familia yake walichangia kumyumbisha sana kijana wao.

Wakawa na shauku kubwa ya kutaka kusikia atawaambia nini. Baada ya salamu, waliingia mpaka sebuleni ambapo Jafet alivunja ukimya na kuwaeleza wazazi wake kilichowafanya wafunge safari ya ghafla asubuhi hiyo.

“Hivi wewe Jafet una akili kweli wewe? Huyu mzee na familia yako si ndiyo waliosababisha ukataka kupoteza maisha kwa maradhi ay figo? Au umesahau? Sikia mzee mwenzangu, kwa mlichomfanyia mwanangu, nakuomba uondoke, mlango ule pale, ondoka haraka kabla hatujakorofishana,” alisema baba yake Jafet huku akisimama kwenye kiti alichokuwa amekaa, watu wote wakabaki kimya kabisa kwa sababu alichokisema baba yake Jafet, japokuwa alikuwa mlevi sana, kilikuwa na maana kubwa.
“Lakini mume wangu, hebu ngoja kwanza, tutumie busara katika hili, nakuomba utulize jazba zako,” alisema mama yake Jafet na kuingilia kati mazungumzo hayo lakini baba yake Jafet hakutaka kusikia la muadhini wala mchota maji.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumatano kwenye gazeti la Risasi Mchanganyiko.

2 Comments

Leave a Comment