×

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 7

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Kilichonifanya nimwangalie sana ni kwamba, huo wimbo aliosema aliwekewa na mume wangu, Bubu Hutaka Kusema mume wangu naye alikuwa akiupenda kupindukia, nikamshangaa sana huyu Tiaki.
“Shemeji,” nilimwita.

“Naam.”
“Mbona sikuelewi?”
ENDELEA NAYO SASA…

“Hunielewi kivipi shemeji. Kukuomba wimbo au?”
“Huo wimbo mume wangu alikuwa akiupenda sana. Lakini pia juisi ya ukwaju, mume wangu alikuwa akiipenda. Sasa nashangaa sana. Kwa nini kila kitu alichokipenda yeye na wewe unakipenda?” Niliamua kumfungukia.

“Aaa! Shemeji! Kwani kupenda wimbo mbona kila mtu anapenda. Sasa akitokea mwingine akapenda kama mwingine kuna matatizo hapo?” Alisema Tiaki, nikakosa jibu la moja kwa moja, nilibaki kimya.

Nilisimama kwenda kumuwekea wimbo huo lakini huku nikiwa na wasiwasi na usalama wangu. Niliamini huenda Tiaki ni jini lililojigeuza binadamu na kuishi na watu mitaani.
Baada ya kumuwekea wimbo huo, Tiaki alitulia kimya akiwa amejiinamia jambo lililozidi kunishangaza, kwani yalikuwa mapozi ya mume wangu wakati akisikiliza nyimbo hizo za enzi hizo.

Basi, niliamua kujiambia akilini kwamba, kwa vile kuna watu wengine majirani, niwe jasiri mpaka nione mwisho wa Tiaki, kwamba ni jini kweli au ni shemeji yangu.
Tulikaa kimya wote mpaka wimbo ukaisha, Tiaki akainua kichwa na kusema:
“Mimi najiandaa kuondoka shemeji.”

“Mbona mapema shemeji?” nilimuuliza tukikutana macho, akaachia tabasamu laini.
“Nooo! Nawahi Mapambano kwenda kununua pweza kabla ya kwenda nyumbani,” alisema.

Aliniogopesha zaidi kwani hakuna chakula ambacho mume wangu alikuwa anakipenda kama pweza. Yeye alikuwa anabeba ‘hotpoti’ mwenyewe mpaka wanakouza na kununua kiasi chake na mchuzi juu.

Kuna wakati mwingine ilikuwa akikuta pweza wameisha, alifunga safari mpaka eneo linaitwa Mapambano anakokujua mwenyewe na kununua.
Nilianza kuingiwa na hisia tofauti sana. Kwamba, huenda Tiaki siyo jini bali ni marehemu mume wangu, bado anaishi kwa siri.

“Kumbe unapenda pweza shemeji? Yaani upo kama marehemu mume wangu. Na yeye alikuwa mpenzi mkubwa wa pweza,” nilimwambia.
Akajibu: “Kama ni hivyo shemeji ujue mumeo hajafa, bado anaishi kwa sababu kuna anayefanya mambo kwa kushabihiana naye. Teh! Teh! Teh!”

Wakati wote huo, mimi wasiwasi moja kwa moja. Nilikuwa nakaa kimachale sana, kwani niliamini angeweza kunidhuru. Mara simu ya wifi ikaingia, nikamwomba Tiaki nikaongee na simu muhimu chumbani, akanikubalia, nikaondoka sebuleni.
Niliingia chumbani, nikapokea:

“Halo wifi, za huko?”
“Njema wifi. Hivi ulionana na kaka Daniel?”
“Hapana. Vipi kwani?”
“Mbona inasemekana amekuja kwako. Kuna jiranii yetu mmoja leo kampigia mama akamwambia amemuona Daniel akija kwako.”

“Mh! Wifi, mbona sijamwona. Kwangu hajaingia. Jirani mwenyewe ni yule siku ile tunaaga mwili hapa nyumbani ukasema ni wa kijijini kwenu?”
“Huyohuyo.”

“Kwa kweli wifi sijamwona shemeji Daniel wala kivuli chake.”
“Au wifi isijekuwa una mambo yako ya siri na Daniel sasa unazuga?”
Nilimuapia wifi kwamba sina siri yoyote na Daniel, zaidi sana huwa nahisi kama kuna akina Daniel wawili.

“Basi angaliaangalia wifi, si ajabu yuko maeneo hayo kweli kuna kitu anakifuatilia. Utaniambia kama kuna lolote lile,” alisema wifi yangu, nikamwambia poa.
Kabla sijatoka chumbani, nilikaa kitandani na kujishika kichwa huku macho yangu yakiwa kwenye mlango. Nilianza kupata uhakika kwamba, Daniel ni Tiaki.

Nilitumia vigezo kwamba, niliambiwa na wifi alipanda basi nililopanda mimi, lakini ndani ya basi hakuwepo. Matokeo yake akaibuka Tiaki na kudai mimi ni shemeji yake.
Pia nilitumia kigezo kwamba, huyo jirani aliyesema amemuona Daniel akiingia nyumbani si ajabu alimuona Tiaki ambaye sasa niliamini ndiye Daniel. Tena Daniel yule feki.

Moyoni nilimwomba Mungu nikisema yatabainika tu. Kama kuna siri iliyojificha, itakuwa hadharani kwa nguvu zake Mungu.

Basi, nilisimama, nikasali sala ya Baba Yetu kisha nikatoka kwenda sebuleni ambapo nilimkuta Tiaki amekaa tu.
“Vipi kwema huko?” Aliniuliza.

“Kwema kabisa,” nilimjibu nikikaa huku nikitamani kumwambia ukweli kuhusu hisia zangu kwake. Nilimpiga jicho moja la hasira, akaangalia pembeni na kusema:
“Kuna mwanamke mmoja jirani na wakwe zako kule kijijini hivi huwa mnaonana? Maana siku zile nilipokuja jamaa alinionesha. Sasa leo wakati nakuja hapa nimemuona pale kwenye kona ya dukani.”

“Mh!” niliguna kwanza.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave a Comment