
JUHUDI za Christian Pulisic kuondoka Chelsea dirisha hili la usajili wa majira ya joto zimezuiwa na klabu hiyo. Winga huyo atasalia klabuni hapo na kupigania nafasi yake chini ya Thomas Tuchel.
Nafasi ya Pulisic ndani ya kikosi cha vigogo hao wa London imeonekana kuwa finyu hasa baada ya klabu hiyo kumsajili mshambuliaji Raheem Sterlin kutokea Manchester City.

Mpaka sasa Christian Pulisic bado hajaanza mechi yoyote msimu huu, huku mechi zake zote alizocheza akitokea benchi. Jambo hili limemfanya atamani kutoka ili aweze kupata muda mwingi wa kucheza jambo litakalomfanya kuwa katika ubora kuelekea kwenye mashindano ya Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya taifa ya Marekani.

Inasemekana moja ya sababu zilizomfanya Pulisic asipendezwe na kitendo cha Chelsea kumzuia kutoka kwa mkopo ni kuona baadhi ya wachezaji wenzake wengine kama Callum Hudson-Odoi ambaye anaelekea katika klabu ya Bayer Leverkusen nchini ujerumani wakifanikiwa kutolewa kwa mkopo kutoka klabuni hapo.
Pulisic alikuwa tayari kuongeza mkataba wake ndani ya Chelsea kabla ya kuondoka. Manchester United na Newcastle ni miongoni mwa klabu ambazo zilikuwa tayari kumchukua mchezaji huyo kwa mkopo.
Imeandikwa: Abdallah Kaputi kwa msaada wa mitandao.