×

Rais Samia: Marufuku Kusaini Mikataba ya Serikali Bila Kushirikisha Mwanasheria Mkuu -Video

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 29 Septemba, 2022.

 

RAIS Samia leo Septemba 29, 2022 amesema mawakili wa Serikali ni ‘jeshi kubwa’ linalotakiwa kulinda uchumi wa Tanzania kwa kutumiia kalamu zao.

Pia, amesema kuanzia sasa ni marufuku kusainiwa mikataba ya Serikali bila kushirikisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Huko nyuma mikataba ilisainiwa bila ofisi ya AG kufahamu na wanapopata tatizo ndio wanaikumbuka ofisi hiyo huku waliosani wamestaafu au wametangulia mbele ya haki.

Rais Samia amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa kuanzishwa chama cha kitaaluma cha mawakili wa Serikali jijini Dodona.

Rais Samia akitembelea mabanda mbalimbali likiwemo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujionea shughuli mbalimbali pamoja na huduma zitolewazo na Ofisi hizo kabla ya kuhutubia na kuzindua Rasmi Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

 

“Nyinyi ndio ‘majeshi wa kulinda uchumi wetu, kisheria uchumi wetu lazima ulindwe, uwekezaji lazima ulindwe, biashara lazima zilindwe na walinzi wa hayo ni nyinyi.

 

“Nyinyi ni walinzi wa kalamu na siyo walinzi wa mabunduki. Ni walinzi wa kalamu na sheria zenu. Kwa hiyo mwende mkalinde uchumi wetu, kihaki kabisa kiuadilifu kabisa ili nchi hii, iweze kupokea wawekezaji wengi zaidi, tuwekeze zaidi, tukuze uchumi masilahi yapatikane,” amesema Rais Samia.

Rais Samia akibonyeza Kitufe kwenye laptop kuzindua mfumo rasmi wa Kieletroniki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAGMIS), nembo ya Ofisi hiyo pamoja na Chama cha Mawakili wa Serikali katika Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 29 Septemba, 2022.

 

“Tukilinda uwekezaji unaowekezwa Tanzania tutakwenda kupanua wigo mpana unaokuza uchumi, wigo mpana wa kukusanya mapato na yale mliolalamikia hapa itakuwa rahisi Serikali kuyatimiza kwenu,” amsema Rais Samia huku akihaidi atawapa fungu waliloomba ili kulinda uwekezaji na kukuza uchumi.

Pia, Rais Samia amewataka mawakili wa Serikali ambao hawajajisajili kwenye daftari la mawakili wa Serikali wakafanye hivyo wakati bado muda upo.

Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali tarehe 29 Septemba, 2022.

 

“Nirudie kwa ambao bado hawajajisajili, basi wahimize wajisajili, vinginevyo baada ya muda kupita hatutawatambua kama ni mawakili wa Serikali.

 

“Itabidi ama watafute sekta nje waingine, ama sijui watapewa msamaha gani na Mwanasheria Mkuu ili waingie tena kama mawakili wa Serikali.

Hadi sasa kwa mujibu wa Rais Samia mawakili wa Serikali ni 2,652 na kuna wengine bado hawajajisajili kwenye daftarri hilo ambalo liko kwa mujibu wa sheria.

 

Pia, Rais Samia alisema amefurahishwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Dk Eliezer Feleshi kwamba chama hicho kipya kitashirikiana na Chama cha Mawakili Tanganyika, (Tanganyika Law Society-TLS) kwa kufanya kazi pamoja.

Leave a Comment