
Mamia ya wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani wamejitokeza katika zoezi la utoaji namba za kukimbilia kwa ajili ya Kilimanjaro International Premium Lager Marathon inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Waandaaji wa mbio hizo wamesema zoezi hilo la siku mbili litahitimishwa kesho Jumapili saa kumi na mbili jioni kwa mkoa wa Dar es Salaam.
“Tumeanza vizuri na ni matumaini yetu kuwa washiriki watazingatia muda uliowekwa ili tuweze kuwahudumia kwa siku mbili hizi kabla hatujahamia Arusha,” alisema msimamizi wa zoezi hilokutoka kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited Rajon Datoo.

Alisema muamko ni mkubwa na wanatarajia pia kuendelea kuuza tiketi kwa ajili yam bio za Grand Malt KM 5 huku usajili kwa ajili ya Kilimanjaro Premium Lager Km 42 na Tigo Kili International Half Marathon ukiwa umefungwa baada ya idadi ya washiriki kutimia mapema mwezi huu.
Alisema baada ya Dar es Salaam, zoezi hilo litahamia Arusha katika hoteli ya Kibo Palace Februari 21 na 22 kuanzia saa nane mchana hadi saa moja jioni.
“Kituo cha mwisho ni Moshi Mjini ambapo zoezi hilo litafanyika Februari 23 (saa sita mchana hadi saa kumi na moja jioni), Februari 24 (kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni) na Februari 25 (kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni) katika uwanja wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MoCU).

Katika hatua nyingine Waandaaji wa mbio hizo wameendelea kusisitiza kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watu wanaodaiwa kuuza tiketi mtandaoni kwa njia isiyo halali. “Watu hawa watachukuliwa hatua za kisheria kwa sababu ni marufuku kuuza tiketi bila idhini ya waandaaji na hata hivyo usajili umeshafungwa,” ilisema taarifa ya waandaaji hao.
Watakaokimbia na namba feki zikiwemo za miaka iliyopita pia watachukuliwa hatua ikiwemo kuondolewa mashindanoni, kufutiwa matokeo na pia kufungiwa kushiriki katika Kilimanjaro Marathon kabisa.
Wadhamini wa mbio hii ni pamoja na Kilimanjaro Premium Lager-42km (Mdhamini Mkuu), Tigo- 21km Half Marathon, Grand Malt – 5Km Fun Run, wadhamini wa meza za majiTPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na wasambazaji maalumu Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles, KK Security na Keys Hotel.
Mbio hizi zinaandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions Limited.