
MIAKA 83, iliyopita yaani June 28, 1940 wakati Taifa la Ufaransa linapitia kipindi kigumu cha uvamizi wa Ujerumani kupitia utawala wa kidikteta, alitokea mwanaume mmoja aliyeitwa Generali Charles De Gaulle.
Huyu kwa wakati huo alikuwa akitambulika kama Waziri wa Ulinzi na Vita wa Ufaransa ambaye licha ya kupoteza maeneo mengi ya Ufaransa mikononi mwa wavamizi wa Kijerumani aligoma kusitisha vita na kusimamia msimamo wake kwamba ni lazima Wafaransa wote katika nafasi zao wasimame kupigana kufa na kupona kulinda ardhi ya nchi yao.
Katika moja ya hotuba zake kwa Wafaransa aliwahi kutoa kauli ambayo imekuja kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa viongozi mbalimbali duniani ambapo, Generali De Gaulle Juni 28, mwaka 1940 alinukuliwa akisema ‘France has lost a battle, but not the war’ akiwa na maana kuwa ni kweli wanapitia kipindi kigumu cha vita na kupoteza maeneo mengi ya nchi yao.

Lakini aliwataka Wananchi wote kutokata tamaa na kupambana kwani kwa wakati huo ‘Ufaransa ilikuwa imepoteza pigano, lakini haijapoteza vita’.
Nimekumbuka historia hii baada ya kuwa na wikiendi ndefu kwa wadau wa michezo hapa nchini na bila shaka kwa Wanasimba, wikiendi ilikuwa ndefu zaidi, bila shaka wapo ambao wana majeraha makubwa kwa kilichotokea.
Kwanini Wikiendi ndefu? kwanza kuanzia Ijumaa mpaka Jumapili kukikuwa na mashindano ya Afrika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kwa vijana wa shule ambapo kwa Tanzania wawakilishi wetu kwa upande wa wasichana Fountain Gate Dodoma Secondary School waliibuka mabingwa na kufuzu kuwakilisha ukanda kwenye mashindano ya Afrika. Hongera nyingi kwao.
Jumamosi Simba walishuka uwanjani kutuwakilisha katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca na kujikuta wakipokea kipigo cha mabao 3-0 kwenye mchezo wa nyumbani uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

Ukipita mitandaoni na vijiwe mbalimbali vya michezo utagundua kuwa wengi wa mashabiki wa Simba ni kama wanaona hakuna matumaini tena na wameingia hofu ya kampeni yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, wapo ambao wanalalamika bila hata kujua wanacholalamikia, wengine wanasema kocha wengine viongozi.
Ni katika wakati kama huu Simba wamenikumbusha kuhusu Generali Charles De Gaulle na Ufaransa yake na kama De Gaulle alivyowakumbusha Wafaransa, naamini Wanasimba pia wanapaswa kukumbushwa kuwa timu yao imepoteza pambano, lakini haijapoteza vita.
Bila kupepesa macho, kupoteza michezo miwili ya kwanza, hususani mchezo dhidi ya Raja nyumbani ni kweli umeharibu hesabu za Simba kwa kiasi kikubwa lakini ikumbukwe Simba bado wana Fainali nne mbele yao ambazo kama watapata matokeo basi watafuzu robo fainali.

Ni muda wa Wanasimba na Watanzania kwa ujumla wake kuwashika mkono wachezaji wa Simba, kuwakumbusha kuwa bado wana nafasi na wanapaswa kuamini hilo, haitakuwa rahisi lakini wanapaswa kuamini katika ndoto yao.
Baada ya huzuni ya Jumamosi, tabasamu lilirejea kwenye nyuso za Watanzania kupitia wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga walituheshimisha kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Asante Yanga, tunaomba mkumbuke kuwa safari ndiyo kwanza imeanza, shangwe lisizidi tukapoteza hesabu. Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema wao wanaamini kazi ndio kwanza imeanza na hakuna kufanya sherehe ya ushindi na TP Mazembe. Tusimamie hapo kama taifa. Go Simba, Go Yanga.
Stori: Joel Thomas