×

MwanaFA CUP 2024 Yaja na Mkakati wa Kuibua na Kuendeleza Vipaji Kwa Vijana

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amewahakikishia vijana na wadau wa mpira wa Miguu katika Wilayani Muheza kuwa atapeleka skauti wa timu kubwa za mpira wa miguu kwenye mashindano ya ngazi ya jimbo ili waweze kuona vipaji ikiwa ni muendelezo wa ajenda ya kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo.
Mhe. Mwinjuma ametoa kauli hiyo  Januari 20, 2024 alipokuwa akigawa seti ya Jezi 132 pamoja na mipira kwa kila Kijiji Wilayani Muheza mkoani Tanga pamoja na kufungua rasmi mashindano ya mpira wa Miguu  yajulikanayo kama MwanaFA Cup
Akizungumzia mashindano ya MwanaFA Cup, Mhe. Mwinjuma amesema mshindi  wa kombe hilo atajishindia shilingi milioni 5 na mshindi wa pili shilingi milioni 3 na mshindi wa Tatu a milioni mbili.
“Lengo letu kama tulivyoelekezwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya Michezo ni kwenda chini kabisa tuhakikishe tunagundua vipaji halafu tuweke jitihada kuvilea, hii itatusaidia kuwa na wachezaji ambao wanaweza hata kuwakilisha Taifa ama wakafanya mpira wa Miguu kuwa ajira yao” amesema.
Ameongeza mashindano hayo yamejikita katika kuvifuata  vipaji katika ngazi ya chini, kuvigundua na kuvipa nafasi ya kuonekana akisisitiza kuwa atahakikisha skauti wa timu kubwa wanafika Wilayani humo timu zitakapofika robo fainali ya mashindano hayo.

Leave a Comment