
mshambuliaji wa Simba, Kibu Dennis maarufu kwa jina la mkandaji amechekelea kutwaa tuzo yake ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara namba nne kwa ubora Afrika baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa KMC Complex.
Ikumbukwe kwamba Machi 14 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba 6-0 Dodoma Jiji ukiwa ni ushindi wa pili mkubwa kwa Simba kupata msimu wa 2024/25 ule wa kwanza ilikuwa Kagera Sugar 2-5 Simba.
Katika mchezo huo Kibu alihusika kwenye mabao manne, alifunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao akachaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo huo walipokomba pointi tatu mazima Simba.
Ni mara ya kwanza Kibu anatwaa tuzo hiyo kwenye ligi huku akifungua akaunti ya mabao ndani ya ligi kwa kuwa mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni Novemba 5 2023 katika mchezo wa Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Kibu amesema kuwa walikuwa wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo na walianza kwa kasi baada ya kupokelewa vizuri na mashabiki jambo ambalo liliwapa nguvu kupambana zaidi.
“Ilikuwa ni mwanzo mzuri hasa ukizingatia kwamba mashabiki walitupokea vizuri na mwisho tukapata ushindi hii ni furaha kwetu. Nimefurahi kupata tuzo kwa kuwa sio kitu chepesi hasa ukizingatia kuna wachezaji zaidi ya 20 walikuwa uwanjani.”
