×

Mwalimu Mkuu Na Walinzi Wakamatwa Wakidaiwa Kumuua Mwanafunzi – Video

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Kagwa iliyopo manispaa ya Sumbawanga aitwaye Novatus Adelhard Mgeni, miaka 15,

Waliokamatwa ni Pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari ST. Kagwa ambaye ni Zacharia Mwasenga, miaka 47. Wengine ni walinzi wawili wa shule hiyo ST. Kagwa ambao ni Michael Donasio, miaka 33 na Geofrey Simon, miaka 30.

Ni kuwa tarehe 23/03/2025 majira ya saa 8:00 usiku watuhumiwa hawa watatu walimshambulia marehemu pamoja na wanafunzi wenzake wawili kwa kuwapiga wakitumia waya.

Hii ilitokana na wanafunzi hao kutuhumiwa kuruka uzio wa ukuta (fence) inayotenganisha shule hizo mbili yaani Kagwa Sekondari na ST. Kagwa Sekondari.

Ilidaiwa wanafunzi hao baada ya kuruka fence waliingia kwenye mabweni ya wasichana.

Wanafunzi hao baada ya kushambuliwa walifikishwa kituo cha Polisi Sumbawanga na hatimaye hospitali ya rufaa ya mkoa Sumbawanga.

Wanafunzi wawili walitibiwa na kuruhusiwa isipokuwa Novatus ambaye hali yake ilizidi kuwa mbaya na hivyo akahamishiwa hospitali ya rufaa ya kanda – Mbeya ambako amefariki akiwa anapatiwa matibabu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linatoa wito kwa walimu na wasimamizi wa shule na taasisi za elimu kutoa adhabu kwa wanafunzi kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyotolewa na wizara ya elimu.