Wachezaji wa timu ya Yanga wakifanya mazoezi.
Hans Mloli, Dar es Salaam
YANGA jeuri mno! Ikiwa kambini kisiwani Pemba imeamua kutangaza kuwa haitarejea siku moja kabla ya mechi yao dhidi ya Azam FC kama ilivyotarajiwa na wengi, badala yake itarejea kutoka visiwani humo zikiwa zimebaki saa chache kabla ya mechi.
Kikosi cha timu ya Azam SC.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, wameamua kufanya hivyo kwa kuwa hawana sababu kubwa ya kuwahi na kwamba wamepanga kumalizia siku zote kwa ajili ya maandalizi na kwamba wakija huku ni kuwavaa wapinzani wao moja kwa moja.
Akizungumzia kuhusu umbali wa safari kuwachosha wachezaji kwa kurejea siku hiyohiyo ya mechi, Muro aliliambia Championi Jumatano kuwa, hakutakuwa na athari zozote kwa kuwa watarejea na ndege yao ya kukodi ambayo itatumia dakika 45 tu hewani kabla ya kutua Dar.
Ameeleza kwamba wanatarajia kutua Dar saa nne asubuhi kabla ya kupumzika kidogo na baadaye kwenda uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
“Maandalizi ni mazuri na tunaendelea vizuri kwa kweli. Tumepanga kurejea huko siku hiyohiyo ya mechi. Tutatua kwenye majira ya saa nne asubuhi hivi, tutapumzika kidogo kisha tutasogea uwanjani kwa ajili ya kuiangamiza Azam, lazima tuifunge tu maana tupo vizuri sana.
“Hakutakuwa na uchovu wowote maana ndege yetu ya kukodi itatumia kama dakika 45 tu kutoka Pemba mpaka Dar, kwa hiyo hakuna tatizo lolote,” alisema Muro.