×

Askari wa Marekani Ashtakiwa kwa Kubeti Operesheni ya Kumkamata Maduro – Video

MWANAJESHI wa kikosi maalum cha Marekani amekamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kutumia taarifa za siri za kijeshi kufanya ubashiri kwenye soko la mtandaoni wakati wa operesheni iliyohusisha kukamatwa kwa aliyekuwa kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro.

Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za Marekani, askari huyo anayefahamika kama Gannon Ken Van Dyke anadaiwa kufanya kuweka dau kupitia jukwaa la ubashiri wa masoko ya matukio lijulikanalo kama Polymarket, akitumia taarifa za ndani kuhusu operesheni ya kijeshi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa Van Dyke aliwekeza dola 33,034 sawa na Tsh 85,929,169 kwenye ubashiri unaohusiana na operesheni hiyo, na baadaye alipata faida ya dola 409,000 sawa na Tsh 1,063,904,779 baada ya matokeo ya tukio hilo kuthibitika.

Mwanajeshi wa kikosi maalum cha Marekani, Gannon Ken Van Dyke

Mamlaka zinasema askari huyo alihusika pia katika kupanga utekelezaji wa operesheni ya kijeshi iliyosababisha kukamatwa kwa Maduro, jambo linaloibua maswali mazito kuhusu matumizi ya taarifa za siri.

Baada ya operesheni hiyo, Van Dyke anadaiwa kupigwa picha akiwa kwenye meli ya kijeshi baharini, akiwa amevaa sare na akiwa na silaha pamoja na wanajeshi wengine.

Idara ya Sheria ya Marekani imemshtaki kwa makosa kadhaa yakiwemo matumizi haramu ya taarifa za serikali, wizi wa taarifa zisizo za umma, ulaghai wa kifedha na miamala haramu ya fedha.

Aidha, Tume ya Biashara ya Marekani (CFTC) pia imefungua mashitaka ya kiraia dhidi yake, ikitaka adhabu kali ikiwemo marufuku ya biashara na faini.

Kampuni ya Polymarket imesema iligundua shughuli hizo na kuziripoti kwa mamlaka husika, ikisisitiza kuwa matumizi ya taarifa za siri katika ubashiri hayakubaliki.

Wakati huo huo, Rais Donald Trump alisema hana taarifa za kina kuhusu tukio hilo lakini alipinga wazo la watu kubashiri matukio ya kisiasa na kijeshi, akisema dunia inazidi kuwa kama “kasino”.

Mamlaka za Marekani zimesema uchunguzi bado unaendelea na hatua zaidi za kisheria zinaweza kuchukuliwa.

Leave a Comment