
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na uchunguzi wa kifo cha mtu ambaye mwili wake ulikutwa ukielea katika maji ya Mto Msimbazi, eneo la Kipawa wilayani Ilala.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Polisi, tukio hilo lilitokea Aprili 30, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri, ambapo mwili huo ulionekana ukielea katika maji yaliyokuwa yakitiririka mtoni humo.
Ilielezwa kuwa mwili huo haukuwa na kichwa, hali iliyozua maswali na kuongeza uzito wa uchunguzi unaoendelea.
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda mwili huo ni wa mtu aitwaye James Temba, mkazi wa Tabata Chang’ombe, wilayani Ilala.
Hata hivyo, Polisi wamesema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho, huku wakisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuhusika.


