
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limepokea taarifa ya kifo cha mwanamke ambaye mwili wake ulikutwa majini katika eneo la daraja la Salender, wilayani Ilala, majira ya saa 4:30 asubuhi ya Mei 11, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mwili huo haukuwa na jeraha lolote la nje. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu anadaiwa kuwa ni Aisha Miraji, mkazi wa Nzasa, Temeke.
Inaelezwa kuwa Mei 10, 2026, marehemu alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na wazazi wake, kufuatia kusumbuliwa na matatizo ya kiafya kwa kipindi cha takribani miaka mitano. Hata hivyo, alitoweka ghafla akiwa hospitalini hapo kabla ya kupatikana kwa mwili wake katika eneo hilo.
Wazazi wa marehemu wameeleza kuwa mtoto wao alikuwa na changamoto za kiafya kwa muda mrefu. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.
