
Benki ya Ushirika Tanzania, Coop Bank Tanzania, imefanya uzinduzi rasmi wa tawi lake jipya mkoani Mtwara, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwasogezea huduma za kifedha wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.
Uzinduzi huo unaashiria kuendelea kupanuka kwa mtandao wa benki hiyo, ambapo kwa sasa Coop Bank Tanzania inafikisha jumla ya matawi matano nchini, yaliyopo Dodoma, Moshi, Tabora, Tandahimba na sasa Mtwara.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Donald Msengi, ameipongeza benki hiyo kwa uamuzi wake wa kupeleka huduma karibu zaidi na wananchi, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa mikopo, huduma za akiba pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi.
Amesema uwepo wa Coop Bank Tanzania utasaidia kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, biashara ndogo na za kati, huku akitoa wito kwa benki hiyo kuendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kuongeza ufanisi wa huduma zake.
Aidha, Donald Msengi amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, ili kuvutia taasisi zaidi za kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Katika hatua nyingine, amewataka viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na AMCOS kufanya kazi kwa weledi na uadilifu, akiwahimiza kuacha vitendo vya kuwadhulumu wakulima pamoja na kukwepa mapato ya serikali, kwani vitendo hivyo vinakwamisha juhudi za maendeleo ya taifa.
Uzinduzi wa tawi hilo unatarajiwa kuongeza fursa za kifedha kwa wananchi wa Mtwara na maeneo ya jirani, na hivyo kusaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.