×

Uchumi wa Russia Waanza Kuyumba, Serikali Yatafuta Njia ya Kuokoa Bajeti, Waziri wa Fedha Afunguka

Waziri wa Fedha wa Russia Anton Siluanov

Wizara ya Fedha ya Russia imeanza kupitia upya bajeti ya mwaka huu na inapanga kupunguza matumizi katika sekta zisizo za ulinzi na huduma za kijamii kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kifedha.

Waziri wa Fedha wa Russia Anton Siluanov amesema serikali inalazimika kufanya tathmini mpya ya matumizi yake kufuatia mabadiliko ya hali ya uchumi, huku akisisitiza kuwa matumizi ya kijeshi na huduma za kijamii yataendelea kuwa kipaumbele kikuu.

Uchumi wa Russia unaendelea kukumbwa na changamoto kubwa kutokana na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kupungua kwa mapato ya mafuta na gesi pamoja na kuongezeka kwa gharama za madeni.

Siluanov amesema matumizi ya bajeti ya serikali kuu yameongezeka kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni. Kati ya mwaka 2019 hadi 2025, matumizi hayo yameongezeka kutoka asilimia 16.6 ya pato la taifa hadi asilimia 20, huku yakiongezeka zaidi ya mara mbili kwa thamani ya fedha.

Aidha, serikali imekuwa ikitegemea akiba ya taifa pamoja na mapato yatokanayo na bidhaa za mafuta kufadhili matumizi hayo, lakini Siluanov ameonya kuwa akiba hizo “hazina ukomo.”

Mchumi Dmitry Polevoy amekadiria kuwa wizara ya fedha inaweza kulazimika kupunguza matumizi kwa kati ya ruble bilioni 300 hadi 700 mwaka huu baada ya kushusha makadirio ya ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 1.2 hadi 0.4.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, nakisi ya bajeti ya Russia ilifikia ruble trilioni 5.8 kati ya Januari na Aprili 2026, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya nakisi iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Katika kipindi hicho, serikali ilitumia ruble trilioni 17.6 huku mapato yakiwa ruble trilioni 11.7 pekee, hali iliyosababisha matumizi kuzidi mapato kwa karibu asilimia 50.

Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa Russia inaweza kulazimika kuongeza kodi mpya au tozo za dharura ili kuziba pengo la bajeti, jambo ambalo linaweza kuongeza mzigo kwa biashara binafsi na wananchi wa kawaida.

Mchumi Kirill Rodionov amesema hakuna njia rahisi ya kuleta uwiano wa bajeti bila kupunguza matumizi makubwa ya serikali, hasa wakati mapato ya mafuta yanapopungua na gharama za vita kuendelea kuongezeka.

Benki ya Gazprombank pia imeonya kuwa serikali italazimika kupata ziada ya mapato kila mwezi ili kufikia malengo yake ya bajeti, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kufikiwa katika mazingira ya sasa ya uchumi.

Leave a Comment