
SERENGETI, MARA – Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imeweka mkakati maalum wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na miradi inakamilika bila kuchelewa.
Akizungumza leo Jumatano, Julai 1, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Sokoine, wilayani Serengeti, mkoani Mara, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tunaanza utekelezaji wa Ilani leo, Ilani ya 2025–2030. Tunaanza utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2026/2027, na pia tunaanza utekelezaji wa Dira mpya ya 2050,” alisema Waziri Mkuu.

Amesema baadhi ya miradi ya maendeleo ilichelewa au kupungua kasi kutokana na uamuzi wa kimkakati wa Serikali kuelekeza rasilimali katika kukamilisha miradi mikubwa ya kitaifa, ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, Daraja la JPM na Reli ya Kisasa (SGR), ambayo sasa imeanza kunufaisha wananchi.
Kuhusu sekta ya miundombinu, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka utaratibu mpya utakaohakikisha fedha za Mfuko wa Barabara zinawafikia moja kwa moja watekelezaji, ili kuondoa ucheleweshaji wa miradi.
“Kuanzia leo, fedha zitakazokusanywa kupitia TRA kwa ajili ya barabara hazitapelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Zitakwenda moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara ili kasi ya ujenzi isiwe ya kusuasua,” alisema.

Amesema hatua hiyo itasaidia wakandarasi kurejea katika maeneo ya kazi na kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali, hususan katika Mkoa wa Mara na maeneo mengine nchini.
“Nimewaelekeza wakandarasi wote waliokuwa wamesimama warudi site. Fedha zitakuwa zinapatikana moja kwa moja kuhakikisha wananchi wananufaika na miundombinu hii muhimu,” aliongeza.
Serikali imesema mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa kasi na kwa ufanisi zaidi.