
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) unalenga kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kuhakikisha amani inaendelea kutawala katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Muliro alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya vyombo vya dola ya kuzuia vitendo vya uhalifu, kuimarisha utulivu na kuwahakikishia wananchi usalama wa maisha na mali zao.
Alisisitiza kuwa ushirikiano huo unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, huku vikosi hivyo vikifanya kazi kwa pamoja katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudumisha amani na utulivu.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu au viashiria vinavyoweza kuhatarisha usalama, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja.