Na Gladness Mallya
KILA mtu ana kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amempatia ili kuendesha maisha yake pamoja na watu wanaomzunguka. Unapozungumzia filamu za Kibongo ni wazi kuwa jina la Steven Kanumba, aliyefariki zaidi ya miaka mitatu iliyopita, bado lina nguvu kubwa.
Kanumba alijaaliwa, siyo tu kipaji cha kuigiza yeye binafsi, bali pia kile cha kuwafundisha wengine, nao wakaonekana mbele za watu. Kuna watu ambao hawakuwahi kufanya maigizo katika vikundi kama vile Kaole au Nyota Ensemble, kama mastaa wengi wa sasa walivyo, lakini wakaibuliwa na Kanumba kabla ya kuja kuwa na majina makubwa.
Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya waigizaji waliopata majina makubwa walipoigiza filamu kwa kubebwa na Kanumba, lakini mara tu baada ya kufariki, spidi yao katika uigizaji imefifia huku wengine wakiamua kuachana kabisa na tasnia hiyo.
JENNIFER
Ni binti aliyekuwa na umri mdogo ambaye alifanya kazi katika filamu kadhaa, lakini hasa aliitendea haki kazi iliyoitwa Uncle JJ ambayo iliandaliwa na Kanumba.
Ni mtoto aliyeonesha kipaji kikubwa cha uigizaji na wengi waliamini angeibuka na kuja kuwa staa mkubwa sana, lakini bahati mbaya, yeye na watoto wenzake ambao pia waliibuliwa na Kanumba ambao ni Sophia na Patrick wamepotea.
Watoto hawa Kanumba alijua namna ya kuwatumia na wote walionesha dalili za kuja kuwa moto wa kuotea mbali lakini ni kama ndoto hiyo imekufa.
UPENDO MUSHI ‘PENDO’
Ni mwanadada aliyeibuka kutoka katika shindano maarufu la Maisha Plus Season 2 na marehemu Kanumba ndiye aliyemshirikisha kwenye filamu zake ikiwemo Ndoa Yangu na ile ya Devil’s Kingdom, ambapo alionesha uwezo mkubwa wa kuigiza.
Alipofariki, msichana huyu alikiri kuwa haamini kama atapata mtu wa kumchezesha filamu kama alivyofanya marehemu aliyeibua kipaji chake. Tangu wakati huo, binti huyo hajaonekana katika kazi yoyote mpya.
Sylvia Shally
Huyu ni Miss Ilala mwaka 2009, ambaye kabla ya kuingia katika uigizaji, aliwahi kuwa mpenzi wa marehemu Kanumba. Alionesha umahiri wake katika Filamu ya Saturday Morning.
Tangu wakati huo, hajawahi kuonekana katika filamu nyingine na habari zinasema, hivi sasa binti huyo ana maisha yake mengine.
Patcho Mwamba
Hakuna mtu aliyeamini kama mwanamuziki huyu nguli wa bendi kubwa ya FM Academia angeweza kuwa muigizaji mzuri. Lakini Kanumba, ambaye alikuwa mmoja wa mashabiki wakubwa wa kundi hilo la Wazee wa Ngwasuma, alikiona kipaji kilichomo ndani ya Patcho.
Alimchukua na kuanza kumtumia katika kazi zake kama vile Devil’s Kingdom na The Shock.
Tangu alipofariki Kanumba, Patcho amepotea kabisa kwenye gemu la filamu kwani haonekani tena katika kazi zingine. Kwa sasa, anaonekana kurejesha makali yake katika kazi yake ya muziki.
Nargis Mohammed
Miss Tanzania huyu namba tatu wa mwaka 2003 hakuwahi kuwa muigizaji kabla ya kuingia mikononi mwa Steven Kanumba.
Baada ya kuwa wapenzi wakati fulani, alicheza pamoja naye filamu kadhaa ikiwemo ile ya Magic House.
Kwa sasa ameipa kisogo kabisa sanaa ya filamu na anaendelea na maisha yake mengine.