
Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), Simba SC na Yanga, wamepata wapinzani wao katika hatua ya awali ya michuano hiyo msimu wa 2026/27.
Simba , maarufu kama Wekundu wa Msimbazi, imepangwa kukutana na Mighty Wanderers ya Malawi katika hatua ya awali ya mashindano hayo. Timu hizo mbili zitachuana kutafuta nafasi ya kusonga mbele hadi raundi ya pili ya hatua ya awali kuelekea kuwania kufuzu hatua ya makundi ya CAFCL.
Kwa upande wa mabingwa wa Tanzania, Yanga, imepangwa kukutana na Gaborone United ya Botswana katika hatua hiyo hiyo ya awali.
Timu zote mbili za Tanzania zitaanza kampeni zao kwa kucheza ugenini kabla ya kumalizia michezo yao ya marudiano nyumbani, hatua ambayo inaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika kuwania nafasi ya kusonga mbele.
Simba na Yanga sasa zitaanza maandalizi ya safari yao ya kimataifa huku zikilenga kuiwakilisha Tanzania vyema na kufikia hatua za juu katika mashindano makubwa ya klabu barani Afrika.