
Jeshi la Polisi limetoa tamko kuhusu sanduku lililokutwa limefungwa kwa kufuli na kutelekezwa katika eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, baada ya tukio hilo kuzua taharuki miongoni mwa wananchi.
Kwa mujibu wa Polisi, taarifa za uwepo wa sanduku hilo zilipokelewa na askari walifika eneo la tukio kwa ajili ya kulikagua na kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.
Baada ya ukaguzi kufanyika kwa kuzingatia taratibu za kiusalama, Polisi walibaini kuwa sanduku hilo halikuwa na kitu chochote kilichokuwa hatari kwa usalama wa wananchi.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa wanapobaini vitu au mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama, huku likisisitiza kuwa ni muhimu kuepuka kugusa au kuhamisha vitu vinavyotia shaka kabla ya vyombo vya usalama kufika eneo husika.
Aidha, Polisi wamewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika eneo hilo ni shwari na wanaendelea kufuatilia matukio mbalimbali ili kuhakikisha usalama unaimarishwa.