×

Trey Songz Atua Dar Kuandika Historia Tamasha la IMBEJU Sauti Moja Kesho

DAR ES SALAAM: Mwimbaji maarufu wa muziki wa R&B kutoka Marekani, Trey Songz, amewasili nchini Tanzania kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha la Imbeju Sauti Moja, huku msanii Diamond Platnumz akiwa miongoni mwa waliompokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Trey Songz amewasili nchini Jumatano, Agosti 12, 2026, akiwa tayari kwa onyesho litakalofanyika Ijumaa, Agosti 14, katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Ujio wa msanii huyo umeongeza hamasa kwa mashabiki wa muziki nchini, ambao wanatarajia kushuhudia burudani kutoka kwa mmoja wa wasanii wanaotambulika katika muziki wa R&B nchini Marekani.

Tamasha la Imbeju Sauti Moja linaandaliwa na CRDB na ni sehemu ya wikiendi maalumu inayounganisha muziki, michezo na uwekezaji katika jamii.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Tully Esther Mwambapa, alisema Trey Songz ni miongoni mwa wasanii wakubwa wa kimataifa watakaotumbuiza katika tukio hilo.

Mbali na Trey Songz, tamasha hilo litakuwa na wasanii wengine wa kimataifa, akiwemo BNXN kutoka Nigeria na Kabza De Small wa Afrika Kusini.

Tanzania pia itawakilishwa na wasanii Mbosso na G Nako, ambao wanatarajiwa kuungana na wageni hao katika kutoa burudani kwa mashabiki.

Trey Songz amejijengea jina kubwa katika muziki wa R&B kupitia kazi mbalimbali zilizopata umaarufu duniani, zikiwemo Bottoms Up, Slow Motion na Say Aah.

Kumpokea kwake jijini Dar es Salaam na Diamond Platnumz kumeongeza mvuto wa ujio wake, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona atakachokileta kwenye jukwaa la Imbeju Sauti Moja.

Kwa sasa, maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea huku macho ya mashabiki yakielekezwa Kijitonyama, ambapo Trey Songz, BNXN, Kabza De Small, Mbosso na G Nako wanatarajiwa kuifanya Ijumaa kuwa usiku wa burudani ya aina yake.

Leave a Comment