
Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) umeingia katika hatua muhimu katika historia ya sekta ya nishati nchini Tanzania, baada ya kufikia uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.
Mradi huo uliopo Rufiji, Mkoa wa Pwani, unatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho, Agosti 22, 2026, katika hafla itakayowakutanisha viongozi pamoja na wadau mbalimbali.
JNHPP umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452, huku ukielezwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya uzalishaji umeme kutekelezwa nchini kwa kutumia fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Nishati, mradi huo tayari umeanza kutoa mchango mkubwa katika Gridi ya Taifa. Katika kipindi kilichoishia Mei 31, 2026, JNHPP ulichangia takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingizwa kwenye gridi.

Uwezo huo unatarajiwa kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme nchini, ambayo yalifikia kiwango cha juu cha takribani MW 2,199.06 Februari 4, 2026.
Mradi wa Julius Nyerere unatarajiwa kuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, pamoja na kusaidia shughuli za uzalishaji, biashara na ukuaji wa uchumi.
Uzinduzi rasmi wa mradi huo kesho unatajwa kuwa hatua muhimu katika historia ya sekta ya nishati Tanzania, huku Serikali ikiendelea kuweka mkazo katika kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha uwezo wa Gridi ya Taifa.

Stori na Anifa Mwegelo | GPL – TUDACO