
Aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza akiwa ndani ya gereza nchini Marekani, miezi kadhaa baada ya kukamatwa na kupelekwa nchini humo.
Picha hizo, ambazo zimeibua gumzo kubwa, zinamuonyesha Maduro akiwa amevalia mavazi ya kijivu huku akiinua mikono yake na kuonyesha ishara ya ushindi.
Hii ni mara ya kwanza kwa umma kumuona akiwa ndani ya Metropolitan Detention Center (MDC) iliyopo Brooklyn, New York, ambako anashikiliwa wakati akiendelea kukabiliwa na mchakato wa kisheria nchini Marekani.
Katika ujumbe ulioambatana na picha hizo kwenye mitandao yake ya kijamii, Maduro amesema yeye pamoja na watu wake wanaendelea kuwa imara. Pia ametoa shukrani kwa familia yake na wafuasi wake kwa maombi pamoja na mshikamano wanaoendelea kumuonyesha.
Hata hivyo, jambo lililozua maswali zaidi ni muda ambao picha hizo zilipigwa na muda zilipotangazwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, picha hizo zinaonekana kuwa zilipigwa Juni 25, 2026, lakini zikawekwa hadharani Agosti 30, 2026, hali ambayo imeongeza mjadala kuhusu mazingira na sababu za kucheleweshwa kwa kuchapishwa kwake.
Maduro kwa sasa anakabiliwa na mashtaka nchini Marekani, ambayo ameyakana, huku kesi yake ikiendelea kufuatiliwa kwa karibu na jumuiya ya kimataifa.
Kuonekana kwake kwa mara ya kwanza akiwa gerezani kumeongeza mjadala kuhusu mustakabali wake wa kisiasa, pamoja na athari ambazo kesi hiyo inaweza kuwa nazo kwa siasa za Venezuela.
Kwa sasa, macho yanaendelea kuelekezwa kwenye hatua zinazofuata za kesi yake nchini Marekani na namna zitakavyoweza kuathiri mustakabali wa Maduro pamoja na hali ya kisiasa nchini Venezuela.
Stori na Mwajabu Abdallah | GPL