
PEMBA: Kampuni ya mawasiliano ya YAS Tanzania imekabidhi vifaa tiba mbalimbali kwa Hospitali ya Wilaya ya Wete Kinyasini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdalla Rashid Ali, ameipongeza kampuni hiyo kwa kujitolea kusaidia jamii kupitia huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema msaada huo utasaidia kuimarisha huduma za afya, hususan kwa akinamama wajawazito wanaofika hospitalini hapo kupata huduma za uzazi, pamoja na kupunguza changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya.

Amesema hatua hiyo inaonesha kuwa YAS si kampuni inayojihusisha na huduma za mawasiliano pekee, bali pia ina dhamira ya kushiriki katika maendeleo ya jamii.
“Nyinyi si watu wa mawasiliano pekee, kumbe mna upande mwingine ambao bado haujajulikana. Leo mmekuja kutuonesha mfano kwa kukabidhi baadhi ya vifaa muhimu kwa hospitali yetu, hususan katika kuwahudumia akinamama wajawazito,” alisema.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema uwekezaji katika afya ya mama na mtoto ni uwekezaji katika maisha ya kizazi kijacho, huku akiwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kampuni ya YAS Zanzibar, Mohamed Wakid, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za afya nchini.
Amesema kupitia kampeni ya Tumaini, kampuni hiyo imeamua kutoa vifaa tiba kwa Hospitali ya Wete Kinyasini ili kusaidia kuboresha huduma za uzazi kwa akinamama wanaofika hospitalini hapo.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo ni ya kipekee kwa kuwa wazo lake lilitokana na wafanyakazi wenyewe wa kampuni hiyo kuguswa na changamoto zinazowakabili akinamama wakati wa kujifungua.
“Kampeni hii ya Tumaini ni ya kipekee, kwani wazo lake limeanzia kwa wafanyakazi wenyewe baada ya kuguswa na changamoto zinazowakabili akinamama wanapofika hospitalini kujifungua,” alisema Wakid.
Akitaja baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa, alisema ni pamoja na vitanda, viti mwendo, vitanda vya kujifungulia, kanga, mashuka na vifaa vingine mbalimbali vinavyohitajika katika utoaji wa huduma za afya.
Aidha, amesema kampuni hiyo imeendelea kupanua huduma zake za mawasiliano Zanzibar, ambapo kwa mujibu wa maelezo yake imefikia takribani asilimia 99 ya wananchi wa visiwa hivyo.
Nao baadhi ya akinamama waliokuwepo hospitalini hapo wameishukuru YAS Tanzania kwa msaada huo, wakisema utasaidia kuboresha mazingira ya huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za uzazi.
Fatma Juma Hamad ameipongeza kampuni hiyo kwa kujitokeza kusaidia hospitali hiyo, huku akizitaka kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuchangia katika kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake, Raya Seif Abdalla amesema vifaa vilivyotolewa vitakuwa na mchango mkubwa katika kusaidia akinamama wanaofika hospitalini hapo kupata huduma wakati wote.
Msaada huo kupitia kampeni ya Tumaini unaonesha mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii nchini Zanzibar.
MWISHO.