×

Netanyahu Aweka Masharti Mazito Kwa Serikali ya Umoja Israel

Chama tawala cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kimeripotiwa kuweka masharti kadhaa ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na chama cha Yashar kinachoongozwa na Gadi Eisenkot, huku kikitaka Netanyahu aendelee kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi chote cha miaka minne bila makubaliano ya kugawana madaraka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Israel, masharti hayo yaliwasilishwa katika mazungumzo yaliyofanyika mapema wiki hii kati ya wawakilishi wa Likud na Yashar kuhusu uwezekano wa kuunda serikali ya umoja.

Kiongozi wa chama hicho, Gadi Eisenkot (katikati), akiwa katika kikao na kiongozi wa chama cha B’Yachad, Naftali Bennett (kushoto), kiongozi wa chama cha Democrats, Yair Golan (wa pili kutoka kushoto), kiongozi wa Yisrael Beytenu, Avigdor Liberman (wa pili kutoka kulia), pamoja na Naibu Kiongozi wa B’Yachad, Yair Lapid, katika Bunge la Israel (Knesset), jijini Jerusalem, Novemba 18, 2026. 

Miongoni mwa masharti hayo ni kutaka vyama vyote vya kisiasa, kuanzia chama cha mrengo mkali wa kulia cha Otzma Yehudit kinachoongozwa na Itamar Ben Gvir hadi chama cha mrengo wa kushoto cha Democrats, viingizwe katika serikali hiyo, isipokuwa vyama viwili vya Kiarabu.

Likud pia inataka washirika wa serikali kuunga mkono mashambulizi mengine dhidi ya Iran, kuendeleza sheria za mageuzi ya mahakama hadi pale makubaliano yatakapofikiwa na kuanzishwa kwa tume ya kisiasa ya kuchunguza shambulizi la Hamas la Oktoba 7, 2023, badala ya tume huru ya uchunguzi wa kitaifa.

Michael Rabello, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya chama cha Likud, akiwasili kwa ajili ya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano na wawakilishi wa chama cha Yashar kinachoongozwa na Gadi Eisenkot, mjini Herzliya, Israel, Novemba 15, 2026. 

Masharti mengine yanahusu kuendelezwa kwa muswada wa kuwataka Wayahudi wa Kiorthodoksi (Haredi) kushiriki katika huduma ya kijeshi, kutobadilishwa kwa masharti ya wafungwa wa Hamas wanaoshikiliwa na Israel pamoja na kutofanyika kwa majeshi ya Israel kujiondoa katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi hilo ndani ya Ukanda wa Gaza hadi tishio la Hamas litakapomalizika.

Aidha, Likud inataka washirika wa serikali kusaini tamko la kupinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina na kutambua Israel kama taifa la watu wa Kiyahudi.

Hata hivyo, haijafahamika wazi namna wawakilishi wa Eisenkot walivyopokea masharti hayo, huku vyanzo vilivyonukuliwa na gazeti la Haaretz vikieleza kuwa mapendekezo hayo hayakuonekana kulenga kuunda serikali ya umoja bali yalikuwa sehemu ya mkakati wa kisiasa wa Netanyahu.

Kwa upande wake, Likud imekanusha baadhi ya taarifa kuhusu masharti hayo, ikisema madai matatu yanayohusu tume ya uchunguzi, mageuzi ya mahakama na huduma ya kijeshi si ya kweli.

Eisenkot, ambaye kwa sasa amepewa jukumu la kujaribu kuunda serikali, amekuwa akipinga kujiunga na serikali inayoongozwa na Netanyahu, ingawa ameonyesha uwezekano wa kushirikiana na Likud katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Wakati huohuo, kiongozi wa chama cha Yisrael Beytenu, Avigdor Liberman, amepinga uwezekano wa kuunda serikali ya wachache itakayohitaji kuungwa mkono na vyama vya Kiarabu vya Ra’am na Joint List, akionya kuwa hatua hiyo inaweza kumsaidia Netanyahu kurejea madarakani akiwa na nguvu zaidi.

Mvutano huo unaonyesha tofauti kubwa za kisiasa zinazokabili mazungumzo ya kuunda serikali mpya nchini Israel, huku masuala ya uongozi, usalama, vita vya Gaza na mustakabali wa taifa la Palestina yakiendelea kuwa vikwazo vikubwa katika kufikia makubaliano.

Leave a Comment