
Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imeirejeshea Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), baada ya kutengua uamuzi wa awali wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliokuwa umeipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0.
Uamuzi huo umetolewa leo, Novemba 24, 2026, kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Senegal kupinga hatua ya CAF ya kubatilisha matokeo ya fainali hiyo na kuipa Morocco ushindi.
Fainali hiyo iliyochezwa Januari 2026 mjini Rabat, Morocco, ilikumbwa na mvutano mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani kwa takribani dakika 15 wakipinga uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti kwa wenyeji katika dakika za mwisho za mchezo.
Hata hivyo, nyota wa Senegal, Sadio Mané, aliwasihi wachezaji wenzake kurejea uwanjani na kuendelea na mchezo. Baada ya kurejea, kipa wa Senegal aliokoa penalti hiyo kabla ya Pape Gueye kufunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza na kuipa timu yake ushindi wa mabao 1-0.
Miezi miwili baadaye, CAF ilitangaza kuibadilisha matokeo ya mchezo huo na kuipa Morocco ushindi wa mezani wa mabao 3-0, ikieleza kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano kwa kuondoka uwanjani.
Hatua hiyo ilipingwa vikali na Senegal, ambayo iliamua kupeleka suala hilo CAS ikitaka haki itendeke na matokeo ya uwanjani yaheshimiwe.
Kupitia uamuzi wake wa leo, CAS imetengua adhabu iliyotolewa na CAF na kurejesha ushindi wa Senegal wa mabao 1-0, hatua inayomaanisha kuwa Simba wa Teranga wamethibitishwa kuwa mabingwa wa AFCON 2025.
Uamuzi huo unamaliza mzozo mkubwa uliotikisa soka la Afrika na kuifanya fainali hiyo kuwa miongoni mwa matukio yenye utata mkubwa katika historia ya mashindano ya AFCON.
Kwa ushindi huo, Senegal inabaki na fahari ya kutwaa taji la Afrika, huku Morocco ikikosa nafasi ya kutwaa ubingwa mbele ya mashabiki wake nyumbani.