
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayozingatia uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha yana nafasi kubwa ya kuvutia ufadhili kutoka kwa kampuni, taasisi na watu binafsi nchini, Benki ya Stanbic Tanzania imesema.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wa mwaka 2026 unaofanyika jijini Dodoma, ambapo suala la kutafuta na kuimarisha vyanzo vya ndani vya fedha limepewa kipaumbele katika majadiliano ya uendelevu wa mashirika hayo.
Benki hiyo, ambayo ni mdhamini wa mkutano huo, imesema mashirika yenye mifumo madhubuti ya kutunza kumbukumbu za fedha na kuonesha namna rasilimali zinavyotumika yana uwezekano mkubwa wa kujenga imani kwa wafadhili wa ndani na kupata fursa zaidi za ufadhili.
Katika kipindi cha siku nne za mkutano huo, kuanzia Novemba 25 hadi 28, wataalamu wa Stanbic wanakutana na wawakilishi wa mashirika hayo kutoa elimu kuhusu namna bora ya kusimamia fedha za miradi, kufanya malipo kwa wafanyakazi na washirika, pamoja na kushughulikia miamala ya fedha za kigeni kwa gharama nafuu na kwa uwazi zaidi.
Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kupitia Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO).
Unaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Mtazamo Mpya kuhusu Uendelevu wa NGOs: Ubunifu, Ushirikiano na Upatikanaji wa Rasilimali za Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani.”
Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 kutoka serikalini, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za Umoja wa Mataifa na washirika wa maendeleo. Kabla ya ufunguzi wake, mashirika 400 yalikuwa yamejisajili kushiriki, yakiwemo Save the Children, ActionAid Tanzania na World Vision Tanzania, pamoja na mitandao ya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Takwimu za Wizara zinaonesha kuwa mashirika 1,066 yasiyo ya kiserikali yalisajiliwa nchini kati ya Julai 2025 na Aprili 2026, yakiwemo 49 ya kimataifa na 973 ya kitaifa.
Huku idadi ya mashirika hayo ikiendelea kuongezeka, mabadiliko na kutokuwa na uhakika kwa upatikanaji wa misaada kutoka nje yameongeza umuhimu wa kutafuta njia mbadala za kugharamia shughuli za maendeleo. Hali hiyo imeifanya NaCoNGO kuweka msisitizo katika ukusanyaji wa rasilimali za ndani, uendelevu wa kifedha na ushirikiano na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Stanbic, wafadhili wa ndani, wakiwemo kampuni, taasisi na taasisi za umma, wanahitaji ushahidi unaoonesha namna fedha wanazotoa zinavyotumika. Hivyo, uwezo wa shirika kutoa taarifa sahihi za mapato na matumizi kwa wakati ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza imani na kuvutia ufadhili endelevu.
Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu za fedha, Makamu wa Rais wa Idara ya Mashirika ya Kimataifa na Sekta ya Umma wa Stanbic Bank Tanzania, Naomi Vicent, amesema uwazi ni msingi wa kujenga uaminifu kati ya mashirika na wafadhili.
“Wafadhili wa ndani huelekeza fedha zao kwa mashirika wanayoyaamini, na uaminifu huo hujengwa kupitia kumbukumbu sahihi za fedha. Shirika linapopokea ruzuku katika akaunti maalumu ya mradi, kufanya malipo yote kwa njia za kidijitali na kuwa na taarifa za fedha zinazopatikana zinapohitajika, linatumia muda mchache kueleza masuala ya fedha na muda mwingi zaidi kutekeleza programu zake,” amesema.
Stanbic imeeleza kuwa huduma zake kwa NGOs, taasisi za kimataifa na za umma zinajumuisha kufungua akaunti tofauti kwa kila mradi au mfadhili ili kuepusha kuchanganya fedha, kufanya malipo ya kidijitali kwa wafanyakazi, wazabuni na wanufaika wa miradi, pamoja na kutoa huduma za mishahara na akaunti binafsi kwa wafanyakazi wa mashirika hayo.
Benki hiyo pia inatoa huduma za kubadilisha fedha za kigeni kwa mashirika yanayopokea ruzuku kwa dola za Marekani au Euro na kutumia fedha hizo katika shughuli zake zinazolipiwa kwa shilingi za Tanzania.
Kupitia Standard Bank Group, mashirika yanayotekeleza miradi katika nchi mbalimbali za Afrika yanaweza pia kupata huduma za kibenki kupitia kundi hilo katika nchi tofauti.
Kwa upande wake, Elias Ngunangwa, Mkuu wa Mahusiano ya Wateja Wakubwa, amesema kampuni nyingi zinazohudumiwa na benki hiyo zinahitaji washirika wa kuaminika katika kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji na ujasiriamali.
Amesema NGOs zenye usimamizi mzuri na mifumo imara ya kifedha zina nafasi nzuri ya kuchaguliwa kutekeleza miradi hiyo, hivyo benki hiyo inalenga kusaidia kujenga mazingira yatakayowaunganisha wafadhili na mashirika kwa misingi ya kuaminiana.
“Lengo letu ni kusaidia pande zote mbili kukutana katika msingi imara ili ufadhili wa ndani ukue na kuwa ushirikiano wa muda mrefu badala ya kuwa msaada wa mara moja,” amesema.
Mkutano huo pia unashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo wizara za Serikali, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, Umoja wa Ulaya, Ubalozi wa Uingereza, Ubalozi wa Uswisi na taasisi za Umoja wa Mataifa.
Ngunangwa ameipongeza Wizara, Ofisi ya Msajili wa NGOs na NaCoNGO kwa kuandaa jukwaa linalowakutanisha Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kupanga kwa pamoja masuala ya maendeleo ya nchi.
Amesema Stanbic imehudumia Tanzania kwa zaidi ya miongo mitatu na inaendelea kujitolea kuchangia ukuaji wa nchi kwa kushirikiana na taasisi zinazohudumia jamii.