×

Lucky: Mbali na uigizaji, mimi ni mkulima mzuri tu

Leo kwenye safu hii tunaye msanii mkongwe, Luckyness Mokiwa ‘Lucky’. Katika maswali 10 aliyoulizwa amefunguka mengi kuhusu maisha pamoja na fani yake ya uigizaji. Ili kujua alichoulizwa na majibu aliyotoa, ungana na Mwandishi Wetu Hamida Hassan aliyefanya naye mahojiano.

Ijumaa: Watu wanasema filamu sasa hivi hazilipi, wewe unasemaje maana naona umewekeza sana kupitia tasnia hiyo?
Lucky: Anayesema hailipi huyo hayupo siriasi na hii kazi, ili kila kitu kiweze kuuzika, lazima kiwe bora. Mimi naamini inalipa na inaweza kuwatoa wengi wakidhamiria.

Ijumaa: Umeshaini sana kwenye filamu ya Identity Card hasa pale ulipocheza kama mlevi, mvutaji wa sigara. Filamu gani nyingine umecheza ambazo watu wamekubali uwezo wako?
Lucky: Nimecheza filamu nyingi hasa kwenye Kampuni ya RJ, ingawa pia nina filamu zangu kama vile Pretty Girl, Bad Luck, Second Wife, Sad Moment pamoja na zile nilizotoa chini ya kampuni yangu ya Lugwa ambazo ni Stuck On You na Mhanga. Zote nimekamua ile mbaya.

Ijumaa: Mbali na uigizaji wa filamu unafanya kazi gani?
Lucky: Mimi ni mfanyabiashara, nalima mazao mbalimbali, pia nafuga kuku. Kwa kifupi mimi ni mkulima mzuri tu.
Ijumaa: Wewe umeolewa, umetulia kwenye ndoa yako, unawazungumziaje mastaa viruka njia ambao wanachangia fani ya uigizaji kuonekana ni kichaka cha ufuska?
Lucky: Unajua wasanii wengine hawajielewi, wanashindwa kutambua kuwa sanaa ni kazi kama kazi nyingine na wengi wao wanaingia kwenye filamu kwa ajili ya kuuza sura na kupata mabwana. Hilo ni tatizo kubwa.
Ijumaa: Ukiwa nyumbani unapenda kumpikia chakula gani mumeo ambacho ukipika anajua hiki kapika mke wangu na anakipenda?
Lucky: Yeye anapenda kupikiwa ugali kuku, hivyo linapokuja suala la kumpikia kiukweli huwa najituma kuhakikisha anafurahi.

Ijumaa: Mumeo akikukera kwa jambo f’lani, ili urudi kwenye hali yako ya kawaida ni mpaka akufanyie nini?
Lucky: Akiniletea midoli anakuwa amenimaliza, napenda sana midoli.
Ijumaa: Kila mwanadamu ana hobi zake, za kwako ni zipi?
Lucky: Napenda sana kuogelea na kusoma vitabu.

Ijumaa: Ni wasanii gani wa nje na wa ndani ambao unapenda uigizaji wao na ungependa kuwa kama wao?
Lucky: Siwezi kuficha, kwa Bongo napenda sana uigizaji wa Riyama Ally, kwa nje nampenda Jackie Appiah wa Ghana.
Ijumaa: Ukipata nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais Magufuli utamwambia nini?
Lucky: Kikubwa nitamuomba yeye na serikali yake waweke utaratibu mzuri wa kulinda kazi zetu.
Ijumaa: Unawashauri nini wasanii wenzako?
Lucky: Wacheze filamu zinazokwenda sambamba na maadili ya Kitanzania, tusikopi wanachofanya Wanigeria, Watanzania tukiamua kucheza tunafunika mataifa mengine.

Leave a Comment