×

Auawa kwa kuchomwa kisu…

MWANZA: Mkazi wa Butuja, Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, Makororo Kitota (26) ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na kifuani akituhumiwa kukutwa na mke wa Pius Pascal.
Tukio hilo lilijiri saa 4: 22 usiku wa Machi 30, mwaka huu kwenye kilabu cha pombe za kienyeji cha JRC kinachomilikiwa na mtu aitwaye Chacha kilichopo Mtaa wa Iloganzala wilayani humu.
Nchama Wanda (33), mkazi wa Sabasaba kwenye manispaa hii, yeye alijeruhiwa tumboni kwa kisu wakati akiamulia ugomvi kati ya marehemu Kitota na Pascal.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Justus Kamugisha, siku ya tukio mtuhumiwa Pascal akiwa kwenye kilabu hicho ulizuka ugomvi kati yake na marehemu akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu na mkewe, Veronica Jonas (33).

Alisema kuwa, uhusiano huo ulisababisha Pascal na mkewe kutengana tangu Agosti, mwaka jana. Lakini siku ya tukio, mwanamke huyo na marehemu walikuwepo kilabuni hapo ambapo ulizuka ugomvi, Pascal akimtuhumu Kitota kuchepuka na mkewe.

Kamanda Kamugisha aliongeza kuwa, katika ugomvi huo, Pascal alimchoma kisu Kitota shingoni na kifuani na kusababisha kifo chake papohapo na pia kumjeruhi tumboni Nchama na kusababisha utumbo kutoka nje.
Alisema Nchama amelezwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza akipatiwa matibabu. Mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Bugando.

Kutokana na mauaji hayo polisi wanamshikilia mke wa mtuhumiwa kwa mahojiano huku mumewe akiwa ametoroka na anatafutwa na polisi.
“Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi la polisi endapo watamuona mtuhumiwa ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Kamugisha.

Leave a Comment