×

Warembo Dar wajiuza jirani na Ubalozi wa Ufaransa

Stori: Issa Mnally na Richard Bukos, Wikienda

Dar es Salaam: Hii ni hatari! Ile Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers, wikiendi iliyopita iliwanasa warembo wanaodaiwa kujihusisha na biashara haramu iliyokatazwa na serikali ya kujiuza wakiwa mita chache kutoka kwenye Ubalozi wa Ufaransa uliopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar, jambo ambalo ni hatari kiusalama.

Kabla ya kuwanasa warembo hao, OFM ilipokea malalamiko ya suala hilo kutoka kwa baadhi ya wakazi wa maeneo hayo ambao walidai kuwa kitendo cha wasichana hao kusimama usiku wa manane na kuuza miili yao maeneo hayo ni hatari kwa ubalozi huo kwani anaweza akaingia mtu mwenye nia mbaya na kusababisha maafa.

“Ni rahisi sana kwa mtu mwenye nia mbaya kupenyeza na kufanya lolote baya,” alisema mmoja wa wakazi hao kwa sharti la kutotajwa jina.

OFM iliweka kambi maeneo hayo ambapo ulipofika usiku mnene, wanawake hao walifika eneo hilo na kuanza biashara hiyo ya ukahaba bila hofu yoyote.

Mara baada ya kupigwa picha, wasichana hao walitoka mbio huku baadhi yao wakikimbilia mawe ambayo wameyaandaa kwa ajili ya kuwarushia wateja wanaowazingua.

Mapema Jumamosi iliyopita, Wikienda lilifika kwenye ubalozi huo na kuulizia kwa walinzi wake kama wana taarifa kuwa kuna wanawake wanajiuza eneo hilo ambapo walisema wao siyo wasemaji na kwamba mwenye mamlaka ya kuzungumza hakuwepo hivyo jitihada za kupata kauli ya ubalozi huo zinaendelea.

Leave a Comment