Said Ally, Dar es Salaam
AZAM FC imeutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esperance de Tunis, jana katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Mchezo huo wa Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho ulikuwa mgumu lakini mabao ya Farid Musa dakika ya 68 na Ramadhani Singano dakika ya 70 yaliiwezesha Azam kupata ushindi huo licha ya wapinzani kutangulia kupata bao lililofungwa na Haithem Jouini dakika ya 33.
Mchezo huo uliokuwa mgumu na kuhudhuriwa na mashabiki wengi wakiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ambao kwa pamoja walikuwa wamevaa jezi za Azam, ulikuwa mgumu kwa timu zote hasa kipindi cha kwanza.
Straika wa Azam, John Bocco alishindwa kutumia nafasi kadhaa za wazi na kama angekuwa makini basi Azam ilikuwa na uwezo wa kupata ushindi mkubwa lakini kukosa kwake umakini kulizidi kuufanya mchezo kuwa mgumu.
Azam ambayo ilimaliza mchezo huo kwa kiungo wake, Jean Mugiranize kupewa kadi ya njano dakika ya 28 kwa kucheza faulo, ilimpoteza beki wake wa kati, Sergie Wawa ambaye aliumia mguu na kutolewa nje dakika ya 89 kisha nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Aprili 19 au 20, mwaka huu, ambapo mshindi wa hapo atafuzu hatua ya mtoano.