ILIPOISHIA: Antony na Matlida ni ndugu waliopoteana wakiwa watoto wadogo. Wanakutana ukubwani na kuanzisha uhusiano wa mapenzi bila kufahamiana lakini baadaye wanajikuta katika maisha magumu yenye changamoto kuliko kawaida kisa uhusiano wao huo.
Mengi yalikwishapita na kila kinachoonekana ni kumbukumbu iliyoendelea kutiririka kichwani kwa Antony mfano wa muvi huku Matlida akiwa amelala kifuani kwake ndani ya kijumba chao cha magunia na miti. Antony anaendelea kukumbuka pia alivyokutana na Thomas kijana aliyemfariji wakati akiwa anagalagala chini kwenye matope akimlilia bibi yake aliyepondwa na jiwe la barafu kichwani.
Teremka nayo…
“Mdogo wangu yuko wapi?” Antony alimuuliza Thomas baada ya kuinua kichwa.
“Yupi?”
“Matlida.”
“Simfahamu!”
“Nilikuwa naye hapa muda si mrefu!”
“Sasa amekwenda wapi?”
“Sijui lakini alikuwepo hapa!”
“Mh!”
“Ndiyo, nisaidie tumtafute.”
“Sawa.”
Thomas alimsaidia Antony akasimama kisha wakaungana na kuendelea kukimbia kwenye mvua hiyo wakiziruka maiti za watu wengi pamoja na mifugo iliyokufa kujaribu kuyaokoa maisha yao lakini wakati wote walipokuwa wanakimbia Antony alikuwa anatazama huku na huko kujaribu kuangaza kama atamuona mdogo wake Matlida.
Hayo yote Antony aliendelea kuyakumbuka akiwa bado amemkumbatia msichana huyo, machozi mengi yakimbubujika, roho ilimuuma mno kutokana na hali halisi ya kimaisha waliyokuwa nayo wakati huo na namna ambavyo mpenzi wake alikuwa amechoka na kuharibika mno usoni kwake.
***
Antony na Matlida walizaliwa mjini Sembu, Kaskazini mwa nchi ya Tanzanibani. Wazazi wao, Bernad Malocha na mkewe Mereciana kwa mara ya kwanza walikutana jijini Kampala, Uganda, ambako wote walikuwa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha David’s Memorial, Bernad akisomea masomo ya Biomedical Engineering (BME) na Mereciana akisomea Laboratory Science and Technology.
“You are so beultiful” (Wewe ni mzuri sana) Bernad alimwamba Mereciana siku moja.
“Sure?” (Kweli?)
“Yes baby, just believe it!” (Ndiyo mpenzi, amini hilo!)
“Ooh! My God! But you are handsome also,” (Ooh! Mungu wangu! Lakini wewe ni mzuri pia).
“Thanks.” (Asante)
Uhusiano wa wawili hao ulizidi kuimarika siku hadi siku, baada ya kumaliza masomo na kupata ajira wote mjini Sembu katika Hospitali ya Rufaa Bugando walianza mipango ya ndoa, Bernad akawataarifu wazazi wake waliokuwa wanaishi Kahama, Shinyanga na Mereciana aliwataarifu wa kwake waliokuwa Arusha.
Kila kitu kikaenda sawa, familia za pande zote zikawasiliana na kufahamiana kisha taratibu za kawaida za ndoa zikafuatia hatimaye zoezi hilo likafanyika huko Sembu, Bernard alikokuwa amejenga nyumba maeneo ya Buswelu.
Maisha yao ya ndoa yalikuwa yenye furaha sana, miaka miwili tu ya kuishi pamoja walifanikiwa kupata mtoto wa kwanza, Antony baadaye Matlida, watoto waliowapenda na kuahidi kutumia nguvu zao zote kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutumia rasilimali zote walizokuwa nazo ili watoto wao wapate elimu bora.
Antony akiwa na umri wa miaka mitano walimuandikisha katika Shule ya Chekechea ya Baptist iliyopo Kona ya Bwiru, hapohapo Sembu alipoingia darasa la kwanza Matlida alikuwa anasoma chekechea katika shule hiyohiyo.
Tofauti na Matlida, Antony hakuwa anafanya vizuri darasani kabisa, miaka miwili alikuwa shuleni lakini uelewa wake wa kunasa vitu darasani ulionekana kuwa chini ambapo wakati dada yake akishika namba moja katika kila mtihani yeye alikuwa anaburuza mkia.
Jambo hilo liliwaumiza sana wazazi wake hasa kutokana na juhudi walizokuwa wanafanya kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora.
“Huyu mtoto sijui ana tatizo gani!” Mereciana alikuwa analalamika kila mara.
“Hata mimi ananishangaza, kichwa chake kimekuwa kizito sana kuelewa.”
“Labda tumuhamishe shule.”
“Mh! Unadhani tatizo ni shule? Mbona Matlida anafanya vizuri na ameanzia hapohapo anaposomea yeye!”
“Tujaribu tuone.”
Hicho ndicho kilichofanyika, wakati Matlida anaingia darasa la kwanza wazazi wake walimuhamisha shule ya Antony akajiunga na Shule ya Msingi Nyakahoja, kuendelea na darasa la pili lakini hata hivyo bado haikusaidia. Namba yake kila mtihani ilikuwa ya kwanza kutoka mwisho, kila mbinu waliyojitahidi kuifanya kumsaidia afanye vizuri iligonga mwamba.
Siku zikazidi kusonga mbele, jambo la kusikitisha zaidi akiwa katika umri huo mdogo Antony alianza kuichukia shule.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz