Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa .
Wilbert Molandi, Dar es Salaam
MARA ya mwisho kwa Taifa Stars kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ni mwaka 1980, tangu hapo Tanzania haijawahi kufuzu kwa michuano hiyo.

Kikosi cha Misri .
Sasa leo Taifa Stars inacheza mechi muhimu ya Kundi G kuwania kufuzu fainali hizo za Afrika mwakani dhidi ya Misri ambayo inahitaji pointi moja tu ili ifuzu.
Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa ametamka kuwa anawaheshimu Misri lakini atahakikisha wachezaji wake leo kwenye Uwanja wa taifa, Dar es Salaam, wanacheza kama mechi ya fainali ili kujiweka pazuri.
Taifa Stars.
Katika Kundi G la kufuzu Afcon 2017 fainali zitakachezwa Gabon, Misri inaongoza ikiwa na pointi saba inafuatia na Nigeria yenye pointi mbili na Taifa Stars inayo moja tu. Chad imejitoa hivyo haina pointi hata moja.
Taifa Stars ikishinda leo, itafikisha pointi nne huku ikiwa na mchezo mmoja dhidi ya Nigeria ambayo haiwezi kufuzu hata ikishinda, hivyo huu ni mchezo muhimu kwa Tanzania.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkwasa alisema maandalizi ya kikosi chake yanatosha kupata ushindi kwenye mchezo huo wa leo na tayari amezinasa mbinu za wapinzani wake.
“Misri wanataka pointi moja tu, hivyo najua watajilinda sana najua watajaza viungo wengi wanaofikia watano kwa ajili ya kuzuia pasi za mwisho kupenya.
“Nimeshafanyia kazi hali hiyo, hatutakubali kuona tunapoteza tukiwa nyumbani, hivyo basi kitu nilichokipanga ni kushambulia lango la wapinzani wetu kwa dakika zote 90.
“Tunaiheshimu Misri, lakini hatutakubali katika mchezo huu tuone tunaupoteza, kikosi changu kipo fiti kwa ajili ya mchezo huo isipokuwa Bocco (John) na Ulimwengu (Thomas) wenye majeraha madogo ambayo hayawezi kuwafanya waikose mechi ya kesho (leo).
“Nimewaambia washambuliaji wangu wafanye jitihada ya kutumia kila nafasi watakayoipata kwa kufunga bao ili tutengeneze mabao mengi,” alisema Mkwasa. Mchezo wa leo utachezeshwa na mwamuzi Eric Otogo-Castane wa Gabon.
Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha wa Misri, Hector Cuper raia wa Argentina hakutaka kuzungumza lolote baada ya mazoezi ya jana jioni ya kikosi chake kwenye Uwanja wa Taifa.
“Kocha hatoweza kuzungumza kwani hali yake si nzuri,” alisema kwa kifupi mmoja wa viongozi wa Misri aliyekuwepo uwanjani hapo. Hata hivyo, Cuper alionekana akiongoza vizuri mazoezi ya timu yake.
Katika mchezo wa leo Taifa Stars, inaweza kuwakilishwa na Aishi Manula, Juma Abdul, Hajji Mwinyi, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
Misri yenyewe itawategemea zaidi nahodha kipa Essam El-Hadary, Ahmed Fathy, Mahmoud Hassan, Amr Gamal, Marwan Mohsen na Mohamed Salah.
