CCM Yaonya Watumishi wa Umma Kuhusu Uwajibikaji na Utoaji Huduma kwa Wananchi – Video

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi, ametoa wito kwa watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utu, nidhamu na matumizi sahihi ya muda katika kuwahudumia wananchi.
Akizungumza mbele ya viongozi wa chama na jumuiya mbalimbali mkoani Dar es Salaam, Kihongosi amesema baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakilalamikia ufuatiliaji wa chama kuhusu miradi ya maendeleo. Ameeleza kuwa malalamiko hayo yanaashiria kutotimiza wajibu ipasavyo na ni kitendo kinachoikosea heshima Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesisitiza kuwa chama hakitaacha kufuatilia utekelezaji wa miradi kwa sababu miradi hiyo ni sehemu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo ndiyo mwongozo wa utekelezaji kwa serikali.
“Kuna baadhi ya watumishi wa umma wanasema chama kinawafuatilia. Waambieni tuna wajibu wa kuwafuata, kwa sababu ilani inayotekelezwa ni yetu. Tutawafuata kila wakati kuhakikisha kazi inafanyika kama ilivyokusudiwa na Rais Dkt. Samia,” amesema Kihongosi.
Aidha, amesisitiza kuwa chama kitaendelea kukagua matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo, ikiwemo vituo vya afya, ili kuondoa uzembe unaoweza kusababisha CCM ionekane haifanyi kazi.

